Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Minziro: Yanga hatujalipwa tangu Februari

17th May 2012
Print
Comments
Kaimu kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa mashindano ya Kombe la Kagame timu ya Yanga, Fred Felix Minziro

Kaimu kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa mashindano ya Kombe la Kagame timu ya Yanga, Fred Felix Minziro, ametishia kujiuzulu nafasi yake hiyo endapo uongozi wa klabu hiyo hautamlipa malimbikizo yake ya mshahara anayodai.

Minziro alieleza jana jijini Dar es Salaam kuwa anadai malimbikizo yake ya mshahara ya kuanzia mwezi Februari mwaka huu.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga amesema kuwa amefikia maamuzi ya kuweka wazi malalamiko yake kutokana na kushindwa kuendelea kuvumilia hali hiyo.

"Uvumilivu umenishinda, umefika kikomo, huwa sipendi kuzungumza lakini sasa nimeamua kuweka wazi, benchi la ufundi nzima linadai na sisi mimi peke yangu," alisema kocha huyo ambaye ndiye aliyeongoza timu wakati inalala magoli 5-0 kutoka kwa watani zao Simba.

Alisema kuwa mambo ndani ya klabu hiyo yamekuwa magumu tangu pale viongozi wao walipoacha kulipa posho kwa wachezaji jambo ambalo lilipunguza morari na kuifanya timu ipate matokeo yasiyoridhisha na hatimaye kupoteza ubingwa waliokuwa wanaushikilia.

Aliongeza kuwa hali hiyo ilitokea pia msimu uliopita ambapo baadhi ya wachezaji walioachwa na kuhama wanadai na msimu huu walikuwa wakielezwa kwamba watalipwa lakini hawakupata chochote hadi msimu umemalizika.

"Programu ya mazoezi ilipangwa ianze Juni Mosi, kama nitakuwa bado sijalipwa madai yangu sitaweza kwenda kuongoza mazoezi, na watakaponilipa kama wataendelea kunihitaji nitafanya kazi na wakinitimua basi nitatafuta timu nyingine, niko tayari kwa lolote," Minziro aliongeza.

Alisema kwamba amechoshwa na ahadi ambapo awali uongozi uliwaahidi utawalipa baada ya mechi ya Klabu Bingwa Afrika ambapo waliikabili Zamalek ya Misri na ahadi nyingine ilikuwa ni baada ya mechi ya watani lakini hadi jana hakuna kilichokuwa kimetekelezwa.

Alisema pia anashangaa kuona tangu ligi ilipomalizika hakuna kikao chochote cha kufanya tathmini kilichofanyika ikiwemo maandalizi ya usajili wakati yeye sasa ndiye mkuu wa benchi la ufundi.

Kocha huyo alisema mbali na mishahara yake ya miezi minne, pia anadai posho za mechi 15 na kuweka wazi kwamba kila mechi hulipwa Sh. 100,000.

Naye kipa wa makocha, Mfaume Athumani, alisema kwamba wachezaji na viongozi wa benchi hilo la ufundi wanaishi katika mazingira magumu kutokana na kukosa haki zao hizo.

Athumani aliwataka viongozi wawalipe na kuendeleza Yanga yao ambayo ni moja na wasiruhusu mpasuko uwepo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alishindwa kuthibitisha au kukataa madai ya Minziro na kuongeza kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu za heshima ya kiutawala.

Mwesigwa alisema kuwa endapo Minziro anaidai klabu anatakiwa awasilishe madai yake ofisini katika njia zinazostahili ili yaweze kutatuliwa. 

NIPASHE ndio lilikuwa gazeti la kwanza kuandika taarifa za aliyekuwa kocha mkuu, Kostadin Papic, kwamba hajalipwa mshahara tangu Februari lakini uongozi wa Yanga ulianza kukanusha mfululizo taarifa hizo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles