Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Rais aliyefungua njia kwa watawala kusimama kizimbani

13th May 2012
Print
Comments
Benjamin Mkapa (wa tatu kutoka kushoto) akisindikizwa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Mei 7, mwaka huu, Tanzania iliingia katika sura mpya ya haki na usawa, baada ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, kusimama kizimbani, akitoa ushahidi.

Historia ya nchi haijaandika mahali popote, kwamba Rais mstaafu ama aliye madarakani baada ya uhuru wa Desemba 9, 1961, aliwahi kusimama kizimbani, kwa kushitakiwa ama kutoa ushahidi.

Hivyo Mkapa alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akiwa shahidi katika shauri la aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, inaleta mabadiliko ya kifikra miongoni mwa jamii.

Kitendo cha Mkapa kusimamishwa kizimbani kinatokana na shauri la uhujumu uchumi linalomkabili Profesa Mahalu, akidaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni 2 katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania mjini Rome huko Italia.

Mkapa akatoa utetezi wake, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Illivin Mgeta, huku akiongozwa na Wakili wa Profesa Mahalu, Alex Mgongolwa.

MITAZAMO TOFAUTI

Je, kuna haja sasa kwa viongozi wakuu wa nchi hususani marais, kufikishwa mahakamani kutoa ushahidi ama (ikibidi) kushitakiwa kwa makosa wanayodaiwa kuyafanya. Ipo mitazamo tofauti inayopaswa kujadiliwa.

Katika kulijadili hilo, kuna hoja nyingi zinaweza kuibuliwa; moja wapo ni kutafakari athari zake katika mwenendo wa shauri husika, pili ni namna anavyopaswa kushiriki shauri lenyewe na tatu nafasi ya matokeo ya shauri kwa aliyewahi kuwa kiongozi.

Hoja hizo na nyingine zinaweza kuibua mjadala mpana zaidi na utakaochukua muda mrefu, lakini itoshe kutathmini athari zikiwemo za kisaikolojia, zinazotokana na kusimama kwa Rais mstaafu kizimbani.

Akiwa sehemu wanayosimama raia wa kawaida ambao hawajawahi kuwa hata Katibu wa Kata, Rais mstaafu anahojiwa kwa kuulizwa maswali, anatii agizo kwa kutekeleza wajibu wake kuyajibu maswali.

Kama ni safari ya haki na usawa, bila shaka Mkapa amekuwa mwanzo mzuri japo kwa kushiriki kutoa ushahidi.

Ukiacha Urais alioushika kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, Mkapa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hadhi hiyo ndani ya chama hicho ni sawa na walivyo wanasiasa kama Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF), Augustino Mrema wa TLP na Freeman Mbowe wa Chadema.

Wanasiasa hao waliowahi kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nyakati tofauti, wamewahi kusimama kizimbani kwa sababu ya kushitakiwa kwa makosa tofauti.

Hivyo ‘picha’ iliyojengeka ni kuona urahisi na uwezekano kwa Mwenyekiti wa chama cha siasa kisichokuwa madarakani, kushitakiwa lakini aliyewahi ama anayeshika nafasi kama hiyo kwa chama tawala haiwezekani.

Ni ukweli ulio wazi kwamba Mwenyekiti wa CCM analindwa na kofia ya urais, inayotoa zuio la kushitakiwa kwa kosa alilolifanya akiwa madarakani.

Ndio maana hata Mkapa aliposimama kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakuwa mshitakiwa.

Alikwenda kama shahidi ambaye sehemu ya maelezo yake alikaririwa akisema;

“Ninafahamu jengo la ubalozi, lilinunuliwa kwa Dola za Marekani milioni 3.097, kwa agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utaratibu wa kununua jengo hilo, nilifahamishwa na aliyekuwa balozi nchini humo, Profesa Mahalu.”

Kisha akasema, “ninamfahamu Profesa Mahalu kama msomi mzuri, mfanyakazi mwadilifu….”

Mkapa hakuishia hapo, akakariliwa akitoa ushahidi na akidai, ningeweza kuzuia ununuzi wa jengo hilo, lakini kwa kuona umuhimu wake nikaruhusu linunuliwe kwa sababu niliona gharama kila wakati kukodi jengo.”

Zipo kauli ambazo Mkapa aliishirikisha mahakama na ambazo zinasubiri chombo hicho cha haki kutoa tafsiri na hatimaye hukumu.

Hapa jambo la msingi si kunukuu kila aina ya kauli aliyoitoa Mkapa, lakini ni kurejea katika hoja ya Rais mstaafu kusimama kizimbani, akiwa huru na kutoa ushirikiano stahiki.

Hakuna amani inayohatarishwa kwa nchi, ikiwa viongozi kama huyo wataendelea kufika mahakamani pindi wanapohitajiwa.

Mkapa ametimiza wajibu wake, ameitikia wito wa mahakama, amekwenda kusimama kizimbani na kutoa ushahidi.

Hali hiyo ni kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa. Lakini swali ni kwamba uwezekano uliotoa mwanya kwa Mkapa kusimama kizimbani akiwa shahidi, hauwezi kurekebishwa kwenye Katiba Mpya kiasi cha kuwashuhudia watawala kufika hapo, ikiwa watafanya makosa?

Jawabu la swali hilo litapatikana kabla ya mwaka 2014 ikiwa azma ya serikali kuwa na Katiba Mpya ifikapo mwaka huo, kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, itafikiwa.

USHAHIDI WA MARAIS

Hata hivyo, ikiwa marais wastaafu wataendelea kufikishwa mahakamani, bado kuna tafsiri tofauti za kisheria zitakazoibuka, isipokuwa kama Katiba na sheria zilizopo vitabadilishwa.

Inaweza kutokea Rais aliyekuwa madarakani akafikishwa kizimbani, hasa kwa kutoa ushahidi, je ushahidi wake utakapodhihirika kuwa ni sehemu ya kosa lililotendwa baada ya mahakama kujiridhisha hivyo, nafasi yake inakuwa ipi?

Kwa maana hadi sasa, kama nilivyoeleza awali, sheria hairuhusu kushitakiwa kwa kiongozi aliyewahi kuwa Rais wa nchi. Inahitaji mjadala.

MUITIKIO WA UMMA

Haiwezekani kukosa watu watakaobeza hatua ya Mkapa kusimama kizimbani, lakini ukweli ni kwamba tukio hilo limeibua picha mpya ya usawa na haki mbele za umma.

Imekubalika kwamba kila raia anaweza kusimama kizimbani. Anaweza kutoa ushahidi, anaweza kujibu maswali, hawezi kudhurika isipokuwa ikiwa kwa uamuzi wa mahakama.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles