Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Milovan: Ubingwa Simba bado

17th April 2012
Print
Comments
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic

Licha ya kuongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, amesema kuwa bado timu yake inakabiliwa na ushindani kwenye mechi zilizobaki ingawa ni kweli kwamba wana nafasi kubwa ya kuwavua ubingwa watani zao Yanga ambao juzi walipokea kichapo cha 3-2 kutoka kwa 'ndugu zao, Toto African.

Simba juzi iliendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Bara baada ya kuifunga Ruvu Shooting goli 1-0 na kufikisha pointi 53 ikiwa ni tofauti ya pointi 10 juu ya watani zao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Cirkovic alisema kuwa mechi zote zilizobaki ni ngumu lakini anachozingatia ni kuona wanapata pointi tatu na kujiimarisha kileleni.

Cirkovic alisema kuwa licha ya wachezaji wake kuwa na uchovu unaotokana na ugumu wa mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho, lakini anawaandaa kupambana ili kufanikisha watatwaa ubingwa wa Bara msimu huu.

"Tunakabiliwa na mechi ngumu na zenye ushindani, ila ninafurahi kuona tunapata pointi tatu licha ya wachezaji kutocheza kama ninavyowaeleza," alisema kocha huyo ambaye alielezea tukio la kuingia uwanjani wakati wa mapumziko juzi kumfuata kiungo, Salum Machaku na kumfokea kutokana na kitendo chake cha kucheza tofauti na maelekezo aliyokuwa anampa.

Kocha huyo alisema kuwa ushindani uliopo wa wachezaji kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza ni jambo linalompa faraja kwamba wanaweza kutimiza malengo yao lakini akaongeza kuwa bado chipukizi wanakabiliwa na wakati mgumu.

"Ni ngumu kumuanzisha Messi (Ramadhan Singano) au Edward (Christopher) wakati Okwi (Emmanuel) na Sunzu (Felix) wapo fiti, umeona leo (jana) Kago (Gervais) ameanza kwa sababu Sunzu ni mgonjwa," Cirkovic aliongeza.

Mbali na Sunzu anayeumwa tumbo na homa, kocha huyo alimtaja beki Nassor Masoud 'Cholo' kuwa pia ana nafasi ndogo ya kucheza katika mechi ya kesho dhidi ya JKT Ruvu kutokana na kuwa mgonjwa.

Simba ambao wanahitaji kushinda mechi zake zilizobaki ili kutwaa ubingwa ndio timu pekee iliyobaki kwenye mashindano ya kimataifa ambapo Aprili 29 itaikaribisha Al Alhy Shandy ya Sudan jijini Dar es Salaam.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment