Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Uamsho 43 wakamatwa Zanzibar

22nd July 2012
Print
Comments

Wakati watu 43 wamekamatwa kwa vurugu na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKU), wametakiwa kujisalimisha polisi baada ya kusababisha vurugu na uharibifu mkubwa wa mali za serikali na watu kuporwa bidhaa visiwani humo.

Tamko hilo limetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Azizi Juma Mohammed, alipokuwa akizungumza na NIPASHE, kufuatia vurugu zilizotokea juzi na Jeshi la Polisi kulazimika kutumia maji ya kuwasha na mabomu kuwatawanya wafuasi wa uamsho Zanzibar.

Aliwataja viongozi wanaotakiwa kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi kuwa ni Mtendaji wa Uamsho Farid Hadi, Naibu Amiri wake Sheikhe Khald Azzani, na viongozi waandamizi akiwemo Sheikh Mussa Juma Issa, Sheikh Mselem Ali na Sheikh Suleiman Haji.

Alisema kwamba viongozi hao wanatakiwa kuripoti katika vituo vya polisi kusaidia uchunguzi wa polisi baada ya kutokea vurugu hizo na kusababisha mali mbali mbali kuharibiwa ikiwemo miundombinu katika Manispaa ya Zanzibar.

Alisema kwamba katika vurugu hizo, watu 43 wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Uamsho wamekamatwa na watafikishwa katika vyombo vya sheria baada ya kukamilika uchunguzi wake.

Aidha alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata vyombo vya usafiri zikiwemo pikipiki na baiskeli na kuwataka watu waliopoteza vyombo vyao kuripoti polisi na vielelezo ili wakabidhiwe mali zao. Alisema kwamba vyombo hivyo vilitelekezwa katika maeneo mbali mbali ikiwemo katika eneo la Mchangani baada ya kutokea vurugu hizo.

Akizungumzia chimbuko la vurugu hizo, alisema kwamba viongozi wa Uamsho waliomba kufanya mhadhara katika eneo la Magomeni Mzalendo lakini kutokana na sababu za kiusalama mkutano huo haukuruhusiwa na vyombo vya dola.

Alisema kumbukumbu za mihadhara ya Uamsho zinaonyesha viongozi wake wamekuwa wakitumia nafasi kubwa ya mikutano yao kukashifu serikali na kueneza chuki dhidi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema viongozi wa serikali wilaya baada ya kupitia maombi ya kufanyika mhadhara huo maombi yao yalikataliwa lakini viongozi hao na wafuasi wao waliamua kukusanyika kwa nguvu katika viwanja vya Malindi na kutaka kufanya mhadhara kwa nguvu katika Viwanja vya Malindi karibu na Msikiti wa Mbuyuni.

Alisema wafuasi wa Uamsho mbali na kuwapinga mawe askari pia walifunga njia kwa kutumia mawe, magari mabovu, kuchoma mipira moto na kukata miti na kutupa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Uamsho Abdalla Said, alisema kwamba wafuasi wa uamsho walikusanyika katika eneo la Msikiti wa Mbuyuni kwa lengo la kusoma dua ya pamoja kuombea watu waliokufa kwa ajali ya meli Julai 17, Mwaka huu.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment