


.jpg)
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara , Lazaro Nyalandu, amekanusha madai ya kuwatishia kwa bastola walinzi geti la kijiji cha Mwanyonye, Wilaya ya Singida, ili apite eneo hilo.
Nyalandu alikanusha madai hayo jana kupitia taarifa aliyoituma kwenye vyombo vya habari na kusema kuwa habari hizo hazina ukweli wowote na ni za kutunga.
Alisema akiwa bungeni alipata taarifa hizo na kwamba wanaofanya hivyo wanaeneza uzushi huo kwa makusudi huku wakijua wanatenda kosa kwa kumsingizia uongo.
Alisema amepakwa matope na serikali na vyombo vyake mkoani Singida, akiwepo Kamanda wa Polisi mkoani humo wameshaangazwa na uongo huo uliotungwa na kupelekwa kwenye vyombo vya habari kwa lengo la kuchafuana kisiasa.
Nyalandu aliwatuhumu viongozi waandamizi wa CCM mkoa wa Singida kuhusika na kupanga na kuueneza uongo na uzushi huo.
“Viongozi hawa wa CCM wanakidhalilisha chama, wanachuki, husuda na fitina zisizoelezeka kwangu,” alilalamika Nyalandu na kuongeza kuwa nia ya yao ni kubomoa viongozi wajasiri na waadilifu ndani ya chama ambao wana lengo la kuleta mageuzi ya kweli na kupinga kubebana pamoja na kupambana na rushwa.
“Napenda kusisitiza kwamba viongozi hao wamefilisika, wamepitwa na wakati, na wanatia aibu nchi yetu sitarudi nyuma katika kuijenga nchi yangu, kupambana na uovu, uongo, rushwa, na nawahakikishia viongozi kama hao popote walipo Singida na kwingineko nchini kwamba mwisho wao umefika,” alisema Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini