Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yondani afichua ya moyoni

27th June 2012
Print
Comments
Kelvin Yondani ‘Vidic’

Siku chache tu baada ya kuanza kujifua katika kikosi cha klabu yake mpya ya Yanga akitokea kwa mahasimu wao wa jadi, Simba, beki Kelvin Yondani ‘Vidic’ amefichua ya moyoni mwake kwa kusema kuwa anachotaka ni kuona timu yake ikipata mafanikio makubwa katika msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza baada ya mazoezi yao ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Kaunda, beki huyo ambaye pia huichezea timu ya taifa (Taifa Stars), alisema kuwa hivi sasa anaendelea kujipanga ili kushirikiana na wenzake na mwishowe kuhakikisha kuwa wanaifanyia Yanga mambo makubwa kwenye msimu ujao wa ligi utakaoanza Septemba Mosi.

Usajili wa Yondani bado unakabiliwa na kiwingu kwani Simba inadai kwamba ni mchezaji wao halali na kwamba anapaswa kuendelea kuwatumikia katika msimu ujao.

Hata hivyo, Yondani amewatoa hofu mashabiki wa timu yake mpya kwa kuema kuwa mkataba pekee anaoujua yeye ni wa Yanga tu; na kamwe  hatakuwa tayari kurudi nyuma kuhusiana na uamuzi wake wa kuchepukia Jangwani akitokea kwa ‘Wekundu wa Msimbazi’.

Akieleza zaidi, Yondani alisema kuwa soka ndio maisha yake na hivyo hatakuwa tayari kuona anajiharibia na hivyo akawataka mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi wowote kuhusiana na uhamisho wake.

"Mimi naenda mbele na soka ndio maisha yangu… najipanga kufanya vizuri na huo mkataba mwingine (Simba) wanaujua wenyewe," alisema beki huyo.

Mchezaji mwingine mpya wa Yanga, kiungo Frank Domayo aliyetoka JKT Ruvu, amesema kwamba hatabweteka na ataendelea kujituma ili kiwango chake kiendelee kuwa cha juu na kujihakikishia nafasi ya kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars.

Domayo ambaye kusajiliwa kwake Yanga kulichangiwa pia na kiwango cha juu alichoonyesha wakati akiichezea Stars, alisema kwamba kujituma ndio siri ya mafanikio na hivyo hatakubali kulewa sifa anazopata baada ya kusajiliwa kwenye klabu hiyo kongwe nchini.

Simon Msuva aliyetua Yanga akitokea Moro United, amesema kwamba hahofii kusotea benchi na badala yake atajituma sana mazoezini na kuonyesha uwezo wake wote ili kocha ashawishike na kumpatia namba kwenye kikosi cha kwanza.

Msuva ambaye aliisaidia timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) katika mashindano ya COSAFA mwaka jana jijini Gaborone, Botswana, alisema kwamba lengo lake ni kucheza soka la kulipwa katika timu za nje ya nchi na hivyo atazidisha juhudi ili akuze kipaji chake.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema jana kuwa sekretarieti ya klabu hiyo inaendelea na vikao ili kufanya maamuzi ya mwisho ya kuchagua jina la atakayekuwa kocha mpya wa timu hiyo.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment