Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Vijana Yanga nao wakutana leo

11th May 2012
Print
Comments

Umoja wa vijana wa klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam umeandaa mkutano wa wanachama vijana utakaofanyika leo kwenye makao makuu ya klabu hiyo kuanzia saa 8:00 mchana kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kipigo cha magoli 5-0 walichokipata Jumapili iliyopita kutoka kwa watani zao Simba.

Akizungumza jana, mwenyekiti wa umoja huo, Bakili Makele, alisema kuwa wameamua kukutana ili kunusuru 'mpasuko' ulioko ndani ya klabu yao kuelekea kwenye kipindi cha usajili na mashindano ya Kombe la Kagame ambao wao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo ya ngazi ya klabu kwa nchi Afrika Mashariki na Kati.

Makele alisema kuwa vijana wameamua kujadili mustakabali wa klabu yao ambapo watazungumzia hali iliyotokea katika msimu mzima wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliomalizika Jumapili ambapo Yanga ilivuliwa ubingwa na kumaliza ikiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Alisema kwamba wanaamini kikao hicho kitawafanya vijana waweze kuwaunganisha viongozi wao ili wafanikishe zoezi la usajili wa wachezaji wake na kujiepushwa na 'aibu' nyingine ya kufungwa kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

"Tunafanya hivi ili Yanga tusiwe kama sinema au vioja katika Kagame, tunataka kuepeuka na kipigo na badala yake tunataka kufarijika," aliongeza mwakilishi huyo wa vijana.

Alisema kwa umoja wao wamekuwa na ushawishi wa aina tofauti kwa kuzungumza na wanachama wenzao ambao hufanikisha usajili wa nyota mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Aliongeza pia wanataka kupanga mipango ya kuhakikisha wachezaji wao nyota hawaikimbii Yanga kwa kusaini mikataba ya kuendelea kuichezea timu hiyo licha ya kukosa tiketi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani.

Alisema kwamba taarifa za kuwepo kwa mkutano huo zimeshapelekwa katika uongozi na endapo leo watazuiwa kuingia kwenye jengo hilo watajipanga na kutafuta ukumbi mwingine lakini hawaamini kama wanaweza kuzuiwa.

Hivi karibu Wazee wa klabu hiyo walifungiwa milango nje na kufanya watumie ukumbi wa Afri Centre kwa ajili ya kutoa taarifa zao kwa umma wa Wana-Yanga.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment