Thursday Feb 11, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Diwani CCM kortini kutishia kuua Mbunge

17th May 2012
Print
Comments

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, jana ililazimika kuongezewa ulinzi wa ziada wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi pamoja na askari kanzu kwa ajili ya kukabiliana na kundi kubwa la wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao walifika mahakamani hapo kuhakikisha diwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nduli katika Manispaa ya Iringa, Idd Chonanga, anapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kutishia kumuua, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Ulinzi huo uliimarishwa katika eneo la Mahakama, baada ya kundi la wafuasi hao kuwasili katika kituo kikuu cha polisi saa 3:00 asubuhi wakisubiri kumshuhudia mtuhumiwa huyo anapandishwa katika karandinga na kupelekwa mahakamani. 

Wafuasi hao tangu juzi walikuwa wakidai kuwa kuna njama za kumlinda diwani huyo asifikishwe mahakamani na kuapa kuwa asiposhitakiwa nguvu ya umma itatumika.

Ili kuepusha uwezekano wa kutokea vurugu, polisi walimwondoa diwani huyo kabla ya saa 3:00 kwa kutumia karandinga na kumpeleka katika eneo la mahakama na kuihifadhiwa hadi saa 5:00 alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka.

Ulinzi wa askari hao katika eneo la kituo cha polisi na eneo la mahakama ulisaidia kuwadhibiti wafuasi hao waliomsindikiza mbunge wao kwa kutembea kwa miguu kuelekea mahakamani.

Baada ya Chonanga kupandishwa kizimbani, alisomewa mashitaka mawili ya kutishia kumuua Mchungaji Msigwa na Diwani wa Kata ya Mivinjeni (Chadema), Frank Nyalusi.

Upande wa mashitaka, ukisoma maelezo yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, Consolatha Singano, ulidai kuwa Mei 14, mwaka huu, mshitakiwa huyo akiwa nje ya ofisi za Manispaa ya Iringa, alitishia kumuua kwa maneno mbunge huyo kinyume cha kifungu cha 89 cha Kanuni ya Adhabu kifungu kidogo cha 2 (a) sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Wakili wa Serikali, Faraja Msuya, alidai kuwa katika kosa la kwanza, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kosa la kutishia kumuua Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa. Katika kosa la pili, Chonanga anashitakiwa kwa kutishia kumuua, Diwani mwenzake wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi.

Mtuhumiwa huyo alikana makosa hayo na mahakama hiyo ilitoa masharti ya dhamana kuwa ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili wenye mali isiyohamishika wakiwa na bondi ya Sh. milioni tano kila mmoja. Sharti lingine ni kuwa na mdhamini ambaye ni mtumishi wa serikali.

Hata hivyo, alishindwa kutimiza sharti la pili la kuwa na mdhamni ambaye ni mtumishi wa serikali na hivyo kukosa dhamana na kupelekwa rumande.

Halimu Singano aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo, walijikusanya katika viwanja vilivyopo mkabala na makaburi ya Mashujaa wakijadili namna watakavyokabiliana na kesi hizo za kujeruhiwa na kutishiwa kuuawa kwa viongozi wao.

Chadema wametangaza kufanya  mkutano mwingine wa hadhara Jumapili wiki hii katika eneo la Nduli ambako kulitokea vurugu na kusababisha watu watatu kujeruhiwa na Mchungaji Msigwa kunusurika kucharangwa mapanga.

Juzi watu wanne wakiwamo watoto watatu wa Diwani Chonanga ambao ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Alex Chonanga (23); Meshack Chonanga (20); Greyson Chonanga (31) na Mussa Mtete (25) walifikishwa katika Mahakakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Iringa kujibu tuhuma za kuwashambulia na kuwajeruhi wanachama watatu wa Chadema waliokuwa katika mkutano wa hadhara eneo la Nduli katika Manispaa ya Iringa.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment