


.jpg)
Sudan ndio timu pekee mwanachama wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) iliyokuwa na mwanzo mzuri katika michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 baada ya kupata ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo).
Timu nyingine za CECAFA zilizocheza juzi hazikupata matokeo mazuri baada ya Tanzania (Taifa Stars) kulala ugenini 2-0 dhidi ya Ivory Coast, Kenya ikashikiliwa nyumbani kwa sare ya 0-0 dhidi ya Malawi, Ethiopia waliocheza ugenini jana dhidi ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' wakawastua wenyeji kwa sare ya 1-1 huku Rwanda inayofundishwa na kocha Milutin Sredojevic 'Micho' aliyewahi kuiongoza Yanga ikipata kipigo kikali cha mabao 4-0 kutoka kwa wenyeji Algeria.
Zambia ndio waliowang'oa Sudan katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2012) kabla ya kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini juzi walijikuta wakizidiwa ambapo wenyeji walitawala katika muda mwingi wa mechi hiyo ya kwanza ya kundi lao la D kabla ya kufunga mabao yote katika kipindi cha pili kupitia kwa Mohamed Tahir na Saifeldin Ali.
Katika mechi nyingine za juzi, Senegal walicharuka kutoka kuwa nyuma na kushinda nyumbani 3-1 dhidi ya Liberia, Morocco wakatoka sare ya 1-1 na Gambia, Tunisia wakashinda 3-1 dhidi ya Equatorial Guinea, Sierra Leone wakashinda 2 1 dhidi ya Cape Verde huku Burkina Faso wakishikiliwa nyumbani na Congo Brazaville kwa sare ya 0-0.
Mshambuliaji Jordan Ayew wa klabu ya Olympique Marseile ya Ufaransa alifunga mabao mawili na kuisaidia Ghana kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Lesotho, Misri waliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Msumbiji, Jamhuri ya Afrika ya Kati wakaibuka kidede4a kwa mabao 2-0 dhidi ya Botswana na Cameroon wakashinda 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mechi nyingine za michuano hiyo ya awali ya Kombe la Dunia zilitarajiwa kuchezwa jana usiku.