


.jpg)
Mamalaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura), imesema bei ya mafuta ya aina ya petroli na dizeli kwa mwezi huu imepungua hadi kufikia asilimia tatu, ambayo imetokana na mabadiliko ya bei la soko la dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jana, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano Ewura, Titus Kaguo, alisema petroli imepungua kutoka Sh. 2,231 ya mwezi uliopita na kufikia Sh. 2,183 kwa lita moja mwezi huu.
Kaguo alisema dizeli imepungua kutoka bei ya Sh. 2,098 ya mwezi uliopita hadi kufikia Sh. 2044 kwa mwezi huu, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki sawa na ile ya mwezi uliopita Sh. 2,068.
Pia, Kaguo alisema gharama za usafirishaji na faida kwa kampuni inayoingiza mafuta nchini imepungua kwa wastani wa Dola 45.36 za Kimarekani kwa tani.
“Kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa ya mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa kupangwa na soko, lakini sisi Ewura tutaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa hiyo ili kuwasaidia wadau wa kufanya maamuzi stahiki katika manunuzi yake,” alisema Kaguo.
Hata hivyo, Kaguo alisema kuna maghala matano ambayo yanahifadhi mafuta lakini yako katika mazingira hatarishi mbayo yanachunguzwa.
“Maghala hayo ni, Mansoor Indistries Ltd na Hass Petroleam Ltd ya jijini Mwanza, NSK Oil Company Ltd, Gapco Tanzania Ltd na Mount Meru Petrolium Ltd zote za jijini Arusha… uchunguzi ukithibitisha kwamba mazingira yataleta madhara kwa maisha ya binadamu yanaweza kufungiwa kabisa au kufutwa moja kwa moja,” alisema Kaguo.