Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanafunzi wapiga walimu kwa manati

27th April 2012
Print
Comments

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanafunzi wa Shule za msingi wilayani hapa wameanzisha utaratibu wa kuwapiga kombeo na manati walimu wao kutokana na kile kilichoelezwa na wanafunzi hao kuwa ni kufuatiliwa nyendo zao kwa karibu na walimu hao, ikiwemo ile tabia ya kutoroka vipindi vya masomo.
 
Wakizungumza na NIPASHE jana katika kijiji cha Igaga B kilicho Kata ya Nchunga wilayani hapa, wakazi wa kijiji hicho walisema mbali ya kombeo na manati, walimu wamekuwa wakitishiwa kuuawa kwa njia za kishirikina hasa wanaonekana kuwafuatilia watoto wanaotoroka shule nyakati za masomo.
 
Akijitolea ushuhuda wa vitendo hivyo, mwalimu John Kija alisema amekuwa katika juhudi za kuwarudisha shule wanafunzi ambao wamekuwa wakitoroka shuleni wakati wa masomo, lakini amekuwa akitishiwa na wazazi wa watoto hao kuwa angeuwawa kwa njia za kishirikina.

“Wazazi wengi hapa Kishapu, hawapendi elimu na wamekuwa wakiwatishia watu ambao wamekuwa katika kampeni ya kuwapeleka watoto shuleni ambao wamekuwa wakitoroka wakati wa masomo, nikiwemo mimi mwenyewe ambaye nimetishiwa kuuwawa kwa njia ya kishirikina,”alisema.

Aliongeza kuwa “Nilikuwa nikiwafuata wanafunzi wanaojificha kwenye minyaa na kuwapeleka shuleni, lakini leo sifanyi hivyo kwa sababu nilipewa onyo la kuuwawa endapo ningeendelea.”
 
Walimu wengine ambao walikataa majina yao kuandikwa gazetini (majina tunayo), walisema wakazi wa wilaya ya Kishapu wanashindwa kuwaandikisha watoto shuleni kutokana na hofu ya kishirikina.

Aidha, walisema baadhi ya watoto walioko mashuleni hivi sasa wamekuwa ni watovu wa nidhamu kiasi cha kujiteng’enezea kombeo na manati ambazo huzitumia kuwachapa walimu.
 
“Kwa hivi sasa hatuwaadhibu watoto, maana tunaogopa kuuwawa kwa njia ya kishirikina lakini pia watoto hawa wamekuwa wakitupiga mawe kwa kombeo na manati ambazo wamekuwa wakija nazo shuleni, kwakweli tunafanya kazi katika mazingira magumu sana na ya kukatisha tamaa, kwa mtindo ni lini kiwango cha elimu kitapanda?” alihoji mmoja wa walimu hao.

Wanakijiji hao walisema mbali ya walimu kupewa adhabu hiyo, hawajawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji.

Wameiomba serikali ya mkoa wa Shinyanga iuagize uongozi wa kijiji hicho ili uweze kuitisha mkutano wa hadhara wa kijiji sanjari na kupata taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji chao.

Waliyasema hayo kijijini hapo kwenye mkutano ulioitishwa na watalaam kutoka Shirika la Kutetea na kuimarisha Demokrasia na Tawala za Kijiji, Kata na Wilaya (ADGL)  lililo na makao yake jijini Mwanza kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kubaini, kujadili na kuchukua hatua kuhusu masuala yanayominya maendeleo na utawala wa demokrasia kwa ngazi hizo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles