


Nilipokuwa mtoto, nikisoma shule ya msingi, nilishiriki kukimbia mchaka-mchaka huku tukiimba nyimbo tofauti.
Asubuhi yenye baridi iliyodumu kipindi kirefu cha mwaka kutokana na mazingira bora yaliyokuwepo, tulikimbia, tuliimba. Moja ya nyimbo ninazozikumbuka ulisema hivi:
“Bandaaa wa Malawi….(ahaaaaa), ametuvalia ngozi ya Simba….(ahaaaaa), kututishia Watanzania…(ahaaaa), Watanzaniaaaa hatujali…(ahaaaa), hatujali mamaaaa, hatujali…ahaaaa)”
Wimbo wenye ubeti huo uliimbwa sehemu kubwa ya nchi, ukiwahusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, waliokuwa wanapitia mafunzo ya mgambo na askari walipokuwa kwenye mazoezi hasa ya viungo kama kukimbia.
Taifa lilisimama kwa wakati huo, likipinga hatua ya aliyekuwa Rais wa Malawi, marehemu Kamuzu Banda aliyefariki Novemba 15, 1997, kutaka eneo lote la Ziwa Nyasa ambalo upande wa pili wanaliita Ziwa Malawi, kuwa mali yao.
Banda hakuishia katika Ziwa hilo tu, bali akasema hata sehemu ya ardhi katika nchi kavu, upande wa mkoa wa Ruvuma, ilikuwa mali ya Malawi. Kituko!
Vituko vya Banda, mwanasiasa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Malawi mwaka 1963 na kuiongoza nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1964, vikazimwa na ujasiri, ushupavu na uimara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hapo ndipo taifa lilipomuunga mkono kwa ujasiri huo, hata ikafikia kuhamasishana kwa kutumia nyimbo ukiwemo niliounukuu hapo juu.
Hivi karibuni, gazeti mtandao la Nyasa Times, likikariri gazeti jingine linalochapishwa nchini Malawi, Daily Times, limemnukuu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa chi hiyo, Patrick Kabambe, akisema Ziwa Nyasa lipo ndani ya Malawi.
Kabambe amekaririwa akisema, msimamo huo upo wazi, kwamba mujibu wa mkataba uliofikiwa mwaka 1890 kati ya Uingereza na Ujerumani (wakoloni), unaoonyesha kuwa mpaka halisi ni eneo la mwisho la Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania!
Kwa maana hiyo, Ziwa Nyasa ambalo kwa karne, miongo, miaka, miezi, wiki, siku, saa, dakika na sekunde, dunia inatambua kwamba sehemu yake ipo ndani ya mipaka ya Tanzania, lihesabike kuwa ni sehemu ya Malawi!
Tanzania ipoteze rasilimali hiyo inayotumika kwa shughuli halali za uvuvi zinazoleta kitoweo, matumizi ya maji na aina nyingine kama utalii wa ndani na nje. Lihamie Malawi!
Kauli na msimamo wa Malawi vinavyofanyika wakati wa utawala wa Rais Joyce Manda aliyeingia madarakani na kuapishwa Aprili 7, mwaka huu, vinanikumbusha ‘vituko’ vya marehemu Banda. Sina hakika kama wa u-ndugu.
Sakata hilo lililofikishwa bungeni, likitakiwa kutolewa ufafanuzi na msimamo wa serikali ya Tanzania, likamuibua Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Akiwa Waziri Mwandamizi aliyekaimu nafasi ya Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, ‘akimshikia’ Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Sitta akawataka Watanzania kuwa na utulivu na kwamba sakata la mpaka huo linashughulikiwa.
Akasema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, atatoa tamko rasmi bungeni kesho (Jumatatu), lakini akaenda mbele zaidi na kulihakikishia Taifa kwamba, Tanzania ipo tayari kwa chokochoko za aina yoyote.
Nilimsikiliza Sitta akieleza hayo, na alipomalizia kuyakinisha kwamba “Tanzania ipo tayari kwa choko choko za aina yoyote’, nilimkumbuka Mwalimu Nyerere.
Nilimkumbuka Mwalimu Nyerere kwa ujasiri usiotiliwa shaka, kwa kusimama juu ya anachokiamini, kwa kutokuwa mnafiki pindi maslahi ya taifa yanapoguswa, yanapotikishwa.
Chokochoko zinazofanywa na Malawi hazihitaji kupata jawabu linalotokana na hofu, woga ama kuwachekea. Kutangaza kuchukua ardhi ya nchi isivyo halali, tena kwa majigambo kama ilivyofanya Malawi ni kejeli inayostahili kukemewa na kutolewa onyo kali kama alivyofanya Sitta. Haina maana kwa hatua hiyo, kwamba nchi inapaswa kuingia vitani…hapana! Wengi tunaamini katika mazungumzo ya kidiplomasia kuwa muarobaini wa kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Lakini Malawi inapoibuka kupitia viongozi wake, na kutangaza azma ya kuichukua ardhi ya Tanzania, hata kama ingekuwa ni yenye ukubwa wa ncha ya ukucha kwenye kidole cha mtoto mchanga, inahitaji ujasiri, inahitaji kusimamia kile unachokiamini, inahitajika kutokuwa mnafiki, bali kukemea. Tanzania inapaswa kuendelea na mchakato wa kidiplomasia, lakini zaidi kujiweka tayari kwa chokochoko za aina yoyote, ili nchi isichezewe na wasiostahili.
Ujasiri aliouonyesha Sitta katika kujibu mzozo wa mpaka huo, ndivyo inavyostahili kuwashughulikia hata waporaji wa rasilimali za umma walio ndani ya nchi.
Ziwa Nyasa ni moja ya rasilimali za umma hivyo hatua ya Malawi kutaka kulichukua, ni uporaji usiotofautiana na uporaji mwingine unaofanyika kwenye fedha za umma, madini, maliasili na nyinginezo.
Waporaji ama wenye nia ya kupora rasilimali za nchi wanapaswa kuambia, Tanzania kupitia serikali yake ipo tayari kwa chokochoko za aina yoyote. Malawi haijapora lakini imepewa karipio la awali. Wapo waporaji walio na wanaoendelea kujineemesha kupitia uporaji wa rasilimali za umma. Wanashughulikiwa kwa namna gani?
Tunahitaji kiongozi wa aina ya Samuel Sitta. Yule ambaye maslahi ya taifa ni zaidi ya misingi ya kidiplomasia, maslahi ya taifa ni zaidi ya ujirani, urafiki ama vinginevyo.
Kinachotakiwa ni kudhibiti vitendo vya uporaji wa rasilimali za umma, uwe unafanywa na mataifa ya nje kama inavyotaka kutokea kwa Malawi ama ndani ya nchi kama ilivyo kwa mafisadi. Hapo ndipo Tanzania yenye neema itakapopatikana.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE.