Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nyongeza nauli daladala zakataliwa

25th May 2012
Print
Comments
Daladala

Wadau wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam wamepinga mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ya kutaka kupandisha nauli za daladala kwa takribani asilimia 150.

Kampuni ya Cordial Transort Service inayosafirisha abiria jijini Dar es Salaam iliwasilisha rasmi mapendekezo yao kwa Sumatra ikiomba nyongeza hiyo ambayo yalidiwa na wadau wa usafirishaji kabla ya kupata baraka za mamlaka hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wamiliki wa Daladala jijini Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabruk, aliwasilisha mapendekezo hayo katika kikao maalum cha wadau jana.

Katika mapendekzeo hayo, kampuni hiyo imeomba safari zinazotozwa nauli ya Sh. 300 zipande hadi Sh. 750, nauli za Sh. 400 zipande na kufikia Sh. 1,000 huku safari ndefu ambazo kwa sasa abiria analipa Sh. 500 ziongezeke hadi kufikia Sh. 1,250.

Aidha, katika mapendekezo yake Mabruk aliitaka Sumatra na wadau wa usafiri kuongeza nauli anayolipa mwanafunzi kwa sasa ya Sh. 150 kwa safari zote hadi kufikia Sh. 375.

Akizungumza katika kikao hicho cha wadau, Katibu wa Baraza la Ushauri na Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu, Oscar Kikoyo, alipinga mapendekezo hayo na kusema kuwa hayakueleza gharama halisi za uendeshaji wa biashara ya usafirishaji.

“Hawa wasafirishaji wameshindwa kuishawishi Sumatra pamoja na wadau kwa nini wanataka nauli zipande na badala yake wamekuja na hesabu za uongo, hivyo hakuna sababu ya mapendekezo yao kukubaliwa,” alisema Kikoyo.

Alisema ili ombi la msafirishaji liweze kukubaliwa ni lazima awasilishe mahesabu yanayoonyesha kwamba faida ya uwekezaji baada ya kutoa kodi imeshuka chini ya asilimia tano.

Alisema usafiri wa daladala unachukua asilimia 43, asilimia sita ni magari ya watu binafsi huku asilimia 51 ya wakazi wa jiji wakiwa wanatembea kwa miguu kwenda na kurudi katika shughuli zao.

Aliongeza kuwa kwa takwimu hizo bado Jiji la Dar es Salaam linahitaji huduma za usafiri kutoka sekta binafsi na kuwataka wamiliki wa mabasi kuweka mikakati itakayowasaidia kuwatoa hapo walipo.

Aidha, alisema maombi hayo yamejaa udanganyifu ikiwemo kusema kwamba mishahara ya madereva ni Sh. 900,000 kwa mwezi badala ya Sh. 300,000 wanazowalipa kwa mujibu wa maelezo ya madereva waliyoyatoa kwa Sumatra.

Katibu huyo alisema kwamba mapendekezo hayo hayawezi kukubaliwa kwa kuwa hayakidhi kanuni za marejeo za viwango vya huduma za Sumatra za mwaka 2009.


Kwa upande wake, Chama cha Kutetea Abiria (Chakuwa) kimesema kwa sasa hakuna sababu ya wasafirishaji kuongeza nauli.

Makamu Mwenyekiti wa Chakuwa, Meja mstaafu L. Simo, alisema kuwa ili kupunguza gharama za wasafirishaji ambazo zinalalamikiwa, kuna haja ya kuwaondoa wapiga debe ambao wanalipwa fedha nyingi kutoka kwa makondakta.

Pia, alisema sare zao ni chafu na hata uvaaji wao siyo wa maadili.

Akifungua kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmed Kilima, aliwaonya wasafirishaji katika mikoa mbalimbali hapa nchini na kuwataka wafanye kazi zao kwa kuzingatia sheria.

Aliwaonya madereva wanaopandisha nauli bila idhini ya Sumatra hususani nyakati za asubuhi na jioni na kusema kwamba mkono wa sheria utawafikia watu wote wanaofanya mchezo huo.

Alisema katika kukabiliana na madereva wakorofi, Sumatra imezifutia leseni za usafirishaji daladala 23 katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na makosa mbalimbali yaakiwemo ya kupandisha nauli kiholela na kukatisha safari.

Kilima alisema Sumatra imewapiga marufuku madereva waliohusika kuendesha chombo chochote mbacho kinasimamiwa na mamlaka hiyo.

Alitaja magari yaliyofutiwa leseni kuwa yalikuwa yanafanya safari zake kati ya Mwenge na Tegeta na Tegeta hadi Mabwepande.

Ikiwa maombi ya kupandishwa kwa nauli hiyo yangekubaliwa abiria wangepaswa kulipa nauli ya Sh. 750 hadi Sh. 1,000. Kwa sasa safari fupi zinatozwa Sh. 300 na ndefu ni Sh. 400.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles