Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tuache kuidhalilisha elimu

18th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Aibu ya kila mwaka ambayo ama sasa imekuwa sehemu ya utaratibu au utamaduni wa kuendesha vyuo vya elimu ya juu juzi ilijitokeza tena kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na St. John's tawi la Dar es Salaam kuvamia ofisi za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) wakifuatilia mikopo yao.

Katika kadhia hiyo, Polisi ambao mabomu yao ya kutoa machozi siku hizi yamekuwa kawaida kufurumushwa dhidi ya raia, waliyafurumusha dhidi ya wanafunzi hao kwa nia ya kuwatawanya.

Wanafunzi hao wake kwa waume walifika katika ofisi za HELSB kuulizia mikopo yao ya tusheni, chakula, utafiti na matumizi mengine ambayo ni haki yao kulipwa ili kuwawezesha kusoma.

Walifikia hatua hiyo baada ya kusubiri bila mafanikio fedha hizo kuingizwa kwenye akaunti zao benki ilihali wenyewe wakiendelea na masomo vyuoni kwao.

Wanafunzi hao siyo kwamba waliambulia mabomu ya machozi tu kutoka polisi walioitwa kuwatawanya, bali pia waliondoka na simanzi nyingine baada ya kuelezwa na Mkurugenzi wa HELSB kuwa akaunti ambayo inatumika kulipa mikopo ya wanafunzi "inasoma ziro" na kwamba hali hiyo inasababisha ishindwe kuendelea kutoa huduma.

Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB kwamba hakuna hata senti moja kwenye akaunti ya mikopo ya wanafunzi ilizua taharuki, kiasi cha wanafunzi kujiapiza kuwa wasingeondoka kwenye ofisi hizo kwa sababu wana hakika fedha zao zipo ila tatizo zinatafunwa na watendaji wa bodi hiyo.

Misimamo hiyo inayokinzana baina ya wanafunzi na Mtendaji Mkuu wa HELSB ilifanya hali ya mambo katika ofisi hizo kuwa tete, hivyo polisi wakaitwa kuwalazimisha kutawanyika.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wanafunzi kuvamia ofisi za HELSB kwa sababu kama hizi, na tuna hakika haitakuwa mara ya mwisho pia kufanya hivyo.

Tunasikitika kuwa usimamizi na uendeshaji wa sekta ya elimu nchini umekuwa wa kubabaisha kwa kiwango cha kutisha.

Mlolongo wa migomo, malalamiko na kila aina ya utendaji wa kutiliwa shaka vimekuwa sehemu ya utendaji wa wenye wajibu wa kusimamia sekta hii. Ni tatizo lililoanza kidogo kidogo lakini sasa tuna ujasiri wa kusema limekuwa janga la taifa.

Katika kundi la wanafunzi waliofika ofisi za HELSB juzi, yupo mmoja alisema hajawahi kuingiziwa fedha kwenye akaunti yake bila kufika ofisi za bodi kupambana.

Imekuwa ni utamaduni, unawakera, kuwapotezea muda na kuongezea shinikizo katika kusoma, lakini wafanye nini? Hii ni aibu ambayo inasikitisha hata kuizungumza.

Serikali inafahamu vilivyo kwamba ni wanafunzi wangapi wamedahiliwa, wangapi wamekubaliwa kupewa mikopo na inajua fika kwamba wanafunzi waliowengi wanategemea mno mikopo hiyo kuendesha maisha yao, lakini ndani ya watendaji wa serikali kuna kutokujali kwa hali ya juu, wapo wanaokaa tu bila kuchukua hatua zozote kuhakikisha kwamba fedha za watoto hawa wa Kitanzania zinapatikana kwa wakati.

Tulipata kusema mara nyingi katika safu hii kwamba taifa hili limejisahau mno katika usimamizi wa elimu, ndiyo maana pamoja na porojo zote zinazotolewa na wanasiasa eti migomo na migogoro katika vyuo vya elimu ya juu inachangiwa na wanasiasa, haingii akilini kwamba kushindwa kuwapatia wanafunzi mikopo yao kwa wakati ambayo hutumia kununua chakula kunahitaji mtu wa kutoka nje kuwachochea kwenda kudai fedha hizo HELSB.

Tulipata kusema huko nyuma, ukitaka kujua taifa fulani ama liko makini katika mambo yake au linajiendea tu ilmradi siku ziende, tazama na kutafakari linavyosimamia sekta ya elimu. Tunachelea kutoa jibu juu ya mustakabali wetu kama taifa kuhusu elimu.

Tunachukua wasaa huu kuzitaka mamlaka zote zinazosimamia elimu ya taifa hili, kuanzia ngazi ya chekechea hadi elimu ya juu, kuacha kulala usingizi, kuacha mzaha, watu wafanye kazi, uwajibikaji uwe dira yao, vinginevyo tunajenga taifa hatari sana huko tuendako.

Ni vizuri kila mwenye dhamana ya kusimamia elimu ya taifa hili akajiuliza swali moja zito, hivi mwanafunzi anayepambana na serikali na vyombo vyake ili apate haki yake ya kusoma siku akibahatika akahitimu na kupata kazi ya kusimamia mambo katika taifa hili, atakuwa amejengwa mtu wa namba gani?

Je, atakua ni mwadilifu au mwenye hasira na roho ya kulipa kisasi kwa kuwa ni majeruhi wa uzembe na kutokuwajibika kwa watawala na kazi yake kubwa itakuwa kupoza kwanza maumivu yake.

Tukisha kuwajenga vijana wetu hivyo leo, hilo taifa la kesho litakuwaje? Tunataka uwajibikaji.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles