Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ukatili dhidi ya watoto ukomeshwe sasa

17th June 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Jana ilikuwa ni Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16, kila mwaka. Siku hii inaadhimishwa kwa Azimio la nchi 51 wanachama wa iliyokuwa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) kukumbuka mauaji ya kinyama waliofanyiwa watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini mwaka 1976.

Ni siku inayoadhimishwa kukumbuka mauaji ya watoto nchini humo wakati wakidai haki zao za msingi. Lengo lingine la maadhimisha haya ni kuwakumbusha wazazi/walezi na jamii kwa ujumla juu ya haki na wajibu wa jamii katika kuwalea watoto.

Aidha, hutoa nafasi ya kuwakumbusha watoto haki na wajibu wao kama watoto katika Taifa. Maadhimisho haya hutoa fursa kwa viongozi mbalimbali nchini kutoa matamko kulaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto ikiwa ni pamoja na unyanyasaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya walezi na wazazi katika maeneo mbalimbani nchini.

Kwa mfano, Mkuu wa wilaya ya Butiama, mkoani Mara, Bi Angelina Mabula, katika maadhimisho ya siku hiyo katika kijiji cha Kwibara kata ya Mugango wilayani humo amekemea vikali unyanyasaji wa watoto wakiwemo walemavu ambao kauli mbiu ya mwaka huu imewalenga ikisisitiza haki kwa watoto walemavu ndani ya jamii yetu.

Akasema wazazi na walezi wanao wajibu wa kuwapa watoto haki zao za kimsingi ikiwa ni utekelezaji wa sera ya mtoto ya Tanzania ya mwaka 2008 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009, kuwalinda na kuwaepusha na mambo yote maovu ikiwemo kuwasikiliza, kuwajali na kuwaendeleza kiroho na kimwili.

Katika maadhimisho kama haya, watoto nao wamekuwa wakitoa rai kwamba wanahitaji kulindwa dhidi ya mambo maovu ikiwemo ukatili, kutelekezwa, kubakwa, kunajisiwa, ukeketaji, ubaguzi wa kijinsia na kufanyishwa kazi ngumu za malipo madogo.

Tukitafakari kwa makini kauli mbiu ya mwaka huu iliyolenga watoto walemavu, ni ukweli ulio dhihiri kuwa kundi hili limepata misukosuko mingi na wakati mwingine jamii ikitizama bila kuchukua hatua zozote.

Wapo watoto wengi kutokana na kasumba ya ubaguzi wa watoto wenye ulemavu hawapelekwi shule. Huu ni ufinyu wa fikra kwani watoto waliobahatika kupelekwa shule wameonyesha maajabu pamoja na ulemavu walio nao.

Mfano mzuri ni wanafunzi wenye ulemavu wa Shule ya Msingi Viziwi Buguruni jijini Dar es Salaam ambao wametoa wito kuitaka jamii kutowabagua watoto walemavu, kwa sababu nao ni sehemu ya jamii inayokubalika. Kwa msaada wa walimu wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao kuadhimisha ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Winfrida Jeremiah, alisema watoto hao wanakosa raha pale wanaposikia walemavu wananyanyaswa na jamii. Ni wito aliotoa wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na Hoteli ya Serena Dar es Salaam.

Jamii inapaswa kulinda watoto na siyo kuona maovu yanafanywa dhidi yao kisha wananyamaza. Wapo watoto ambao wamezaliwa na ulemavu lakini wengine, ambao ndio wengi wanapata vilema, tena vinavyosababishwa na wazazi au walezi walo.

Ukienda mahospitalini utakuta watoto walioumizwa na wazazi au walezi kwa kupigwa na wengine kwa kuunguzwa moto sehemu mbalimbali za miili yao. Ukiuliza sababu ya ukatili huo unaambiwa kadokoa nyama, kaiba sh.500 na kadhalika. Badala ya kumkanya na kumuelimisha, unamtia majeraha mabaya.

Hii siyo sawa hata kidogo. Hata Umoja wa Mataifa mwaka 1992 ulipitisha Azimio lililosisitiza Haki na Maendeleo ya Mtoto katika kulindwa, kutunzwa, kusomeshwa na kuthaminiwa utu wake, azimio ambalo Tanzania pia iliridhia.

Ni vema serikali sasa itilie mkazo ulinzi wa watoto kwa kuzielekeza mamlaka husika na maendeleo ya watoto, asasi za kijamii na jamii yenyewe kwa ujumla kulisimamia kulilinda na kuliendeleza kundi hili kwa ustawi wa taifa la baadaye.

Ukatili dhidi ya watoto utokomezwe sasa na wale wote wanaobainika kusababisha madhara kwa watoto wetu wachukuliwe hatua stahiki hasa kwa kuzingatia kwamba tunayo sheria ya watoto ya mwaka 2009 ambayo imetoa adhabu kali kwa wahusika.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment