Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Marais EAC wataka Sudan na Sudan ya Kusini wazungumze

29th April 2012
Print
Comments

Marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wametaka vita kati ya nchi za Sudan na Sudan ya Kusini kukomeshwa na nchi hizo zirejee katika meza ya mazungumzo.

Marais, Jakaya Kikwete wa Tanzania, Mwai Kibaki wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda na Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi Therence Sinunguruza wameeleza kusikitishwa kwao na mgogoro wa nchi za Sudan.

“Tunawaasa viongozi wa nchi hizo mbili warudi katika meza ya mazungumzo na kutafuta njia ya amani ya kumaliza masuala yaliyobaki katika mkataba wa amani,” wakuu hao wa nchi walisema katika taarifa ya pamoja.

Hata hivyo, wamesema kuwa wataendelea na wajibu wao wa kutafuta amani katika nchi hizo mbili na zingine zinazopakana na nchi zinazounda jumuiya hiyo.

Katika hatua nyingine wakuu wa nchi pia wameagiza Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza zoezi la uhakiki wa maombi ya Sudan ya Kusini ambayo imeomba kujiunga na jumuiya hiyo.

“Tunalitaka baraza la mawaziri liharakishe zoezi la uhakiki wa maombi ya Sudan ya Kusini ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na lilete taarifa katika mkutano ujao mwezi wa Novemba, mwaka huu” inasomeka sehemu ya taarifa ya wakuu wa nchi.

Mkutano huo pia umeshuhudia itifaki ya masuala ya ushirikiano wa ulinzi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ambapo hivi sasa nchi moja ikivamiwa nchi zote za jumuiya zitashirikiana katika vita hiyo.

Hivi sasa itifaki hiyo itatakiwa kuridhiwa na mabunge ya nchi wanachama ifikapo Novemba 30, mwaka huu na baada ya hapo utakuwa mkataba utakaozilazimu nchi hizo kushirikiana masuala hayo ya ulinzi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles