Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kikongwe ajitia kitanzi kukwepa kuuawa

13th May 2012
Print
Comments

Mfululizo wa mauaji ya wazee wilayani Geita mkoa wa Simiyu, umemlazimisha mzee Hassan Salehe (70) kujitia kitanzi kukwepa kuuawa na wanavijiji wanaoamini ushirikina.

Hivi karibuni vikongwe wanne waliouawa kwa kupigwa kwa mawe na miili yao kuchomwa moto na wanakijiji cha Lwezera wilayani Geita, kwa madai ya kufuga fisi kwenye makazi yao.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lwezera Francis Kadilo aliiambia NIPASHE Jumapili kuwa tukio la kujinyonga kwa kikongwe huyo lilitokea siku moja baada ya vurugu na mauaji vikongwe wenzake na nyumba zao zaidi ya 15 kuteketezwa.

Wazee hao waliuawa kwa madai kuwa walikuwa wakifuga fisi ambao siku hiyo walikula mwanafunzi wa shule ya msingi kijijini hapo. Marehemu Salehe alidaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba za katani na kujitundika kwenye mti umbali wa mita moja kutoka kwenye nyumba yake anayoishi na mwili wake ulionekana juzi saa 2:30 asubuhi.

Lakini Kadilo alionyesha wasiwasi kuwa huenda marehemu alinyongwa maana alivyokuwa amening’ania kwenye mti siyo hali ya kawaida pengine aliuawa na katundikwa kwenye mti.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Deusdedit Nsimike alisema hana taarifa za kifo hicho na kuahidi kutoa taarifa kwa maelezo kuwa amewatuma askari kufuatilia tukio la mauaji ya vikongwe wanne pamoja na kuchunguza tukio la pili la kikongwe huyo aliyejinyonga.

Aidha Nsimike alisema watuhumiwa 26 wamekamatwa na polisi kwenye operesheni inayoendelea ya kuwasaka waliohusika katika mauaji ya vikongwe wanne yaliyotokea wiki iliyopita.

Wakati huo huo Leah Mgogo, anaripoti kutoka Chato, kuwa mama na mwanaye wanakijiji cha Mkuyuni wilayani Chato mkoani Kagera wameuawa kikatili baada ya kunyongwa shingo.

Miili ya mwanamke huyo Judith Johemari (26) na mwanaye Mangelina Boniface (4) ilikutwa nyumbani kwao kwenye chumba alichokuwa amepanga wakati huo akijishughulisha na kilimo kijijini hapo. Ilidaiwa waliuawa saa 7.00 usiku wa kuamkia Jumamosi baada ya wauaji ambao hawajafahamika kuwavamia na kuwanyonga kikatili na kukimbilia kusikojulikana.

Taarifa za awali kutoka kwa majirani zilidai kuwa kabla ya kifo marehemu hao walikuwa pamoja wakizungumza hadi saa 2.30 usiku muda ambao waliingia ndani na kulala.

Majirani hao walidai kuwa asubuhi walishangaa kukuta mlango wa nyumba ya marehemu hao ukiwa wazi na miili ya mama na mwanaye iliyonyongwa shingo hadi kugeuzwa upande wa mwingine ikiwa ndani ya chumba hicho.

Mamia ya wanakijiji walifika nyumbani kwa marehemu hao kushuhudia kabla polisi kuondoa miili yao ili kuifanyia uchunguzi katika hospitali ya Wilaya ya Chato.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Henry Salewi, alithibitisha mauaji hayo na kusema chanzo chake hakijafahamika na uchunguzi unafanyika.

Alisema uchunguzi wa daktari ulibaini kuwa marehemu hao hawakufanyiwa kitendo kingine mbali na kunyongwa hadi kufa.

Salewi alisema pembeni ya miili hiyo kulikutwa sufuria iliyokuwa na kitoweo cha nyama iliyopikwa ambayo wawili hao walikula kabla ya kuuawa .

Aliahidi kuwa polisi itafanya uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini waliowaua wanafamilia hao.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment