Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

HAT kutafiti athari za utoaji leseni kwa sekta ya utalii

13th March 2012
Print
Comments

Shirikisho la Wenye Mahoteli (HAT), limepata fedha kutoka asasi ya Uboreshaji wa Mazingira ya Kibiashara Kitengo cha ushawishi ( (Best-AC) kufanya utafiti wa miezi miwili kuhusu athari za kisheria na uchumi kwa utoaji wa leseni za utalii hapa nchini.

“Ni muhimu kutazama upya namna ya utoaji leseni ili kuwawezesha wajasiriamali wengine washiriki kikamilifu katika kuboresha sekta ya utalii nchini," alisema Mwenyekiti Shirikisho la wenye Mahoteli, Damasi Mfugale.

Alisema ada za leseni ni kubwa mno kwa wananchi wengi wa Tanzania  kushiriki kikamilifu katika kukuza sekta hiyo.

Leseni za utalii Tanzania hutolewa na Bodi ya Leseni za Utalii (TTLB)  ambayo zamani ilikuwa inajulikana kama wakala wa utoaji leseni za utalii  Tanzania (Tala).

Ili kufanikisha kazi hiyo, HAT imewateua washauri wawili, mwanasheria na mchumi ili kuangalia mambo mbalimbali ikiwamo ya ulinganifu na  yanayofanyika katika nchi za Kenya, Uganda, Botswana na Mauritius kuhusiana na masuala ya leseni na kuangalia ni kwa namna gani muundo wa leseni wa sasa unaisaidia Tanzania.

Mwanaharakati na mshauri wa masuala ya sheria ya makampuni, Dk. Eve Hawa Sinare, ataangalia masuala ya kisheria, historia yake, mantiki yake na inavyojitosheleza.

Atakayeshughulikia masuala ya uchumi ni Malcolm Toland.

Ofisa Mtendaji Mkuu  wa HAT , Lidwien Appels,  alisema suala la utoaji leseni la TTLB linahitaji kuangaliwa kwa makini na watoa maamuzi na hivyo  kuwapo na haja ya kufanya utafiti kujua athari zake kisheria na kiuchumi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment