Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Cirkovic: Yanga hawaponi Jumamosi

1st May 2012
Print
Comments
kocha wa Simba, Milovan Cirkovic

Baada ya kuichapa Al Ahly Shandy ya Sudan magoli 3-0 juzi katika mechi ya awali ya hatua ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho, kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kuwa hizo ni salamu kwa wapinzani wao Yanga ambao watakutana Jumamosi katika mechi ya kufunga msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo Simba ambayo ina pointi 59 inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Akizungumza jana, Mserbia Cirkovic alisema kuwa ushindi walioupata dhidi ya Shandy umewapa wachezaji wake ari kubwa ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo ya watani wa jadi.

Cirkovic alisema kuwa anakiamini kikosi chake kwamba kina uwezo wa kuendeleza wimbi la ushindi na kuthibitisha kwamba wao ndio timu bora msimu huu kama inavyofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa wanayoshiriki.

Kocha huyo alisema kwamba Simba iko kwenye kiwango bora na anachotaka kukifanya sasa ni kuona inaendelea kufanya mazoezi ya 'nguvu' kwa kurekebisha makosa yaliyopo.

"Ninaamini tutafanya vizuri na tutaifunga Yanga Jumamosi, matokeo haya yametuweka kwenye nafasi nzuri ya mechi hiyo ya ligi," alitamba Mserbia huyo.

Wakati huo huo, mechi yao ya juzi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza jumla ya Sh. milioni 216.

Katika hatua nyingine vinara hao wa ligi jana mchana waliondoka jijini Dar es Salaam na kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na mechi yao ya watani wa jadi na ile ya marudiano dhidi ya Al Ahly Shandy.

Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Goefrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa kwa sasa Simba iko makini na inataka kuona haipotezi mechi yoyote iliyoko mbele yao.

Kaburu aliongeza kuwa wanawapongeza wanachama na mashabiki wa Simba ambao wamekuwa pamoja kuhakikisha timu yao inafanya vizuri katika mechi za ligi ya Bara na za kimataifa.

Habari zaidi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinasema kuwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) huenda likaipelekea mechi ya marudiano kati ya Simba na Shandy nje ya Sudan endapo haitajiridhisha na usalama uliopo Sudan ambako kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles