Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Membe amshukia Kitine

10th May 2012
Print
Comments
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amemfananisha mwanasiasa mkongwe nchini, Dk. Hassy Kitine, kuwa ni sawa na mganga wa kienyeji kazi yake kubwa ikiwa ni kupika majungu na kuwachonganisha watu.

Membe alitoa kauli hiyo kali jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari alioitisha kungumzia suala la mgogoro wa Morocco na Sahara Magharibi, lakini akaulizwa maswali juu ya siasa za kusaka urais nchini.

Membe alitakiwa atoe msimamo wake juu ya kauli ya Dk. Kitine ambaye alipata kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, waziri, mkuu wa mkoa na mbunge wa Makete, aliyoitoa katika mahojiano na kipindi kimoja cha televisheni nchini akidai kuwa waziri mmoja anajiandaa kugombea urais mwaka 2015 na kwamba anamiliki hoteli kubwa nchini Libya ingawa hakumtaja jina moja kwa moja.

Membe alimfananisha Dk. Kitine na Kigwendu ambaye ni mganga wa kienyeji kazi yake ikiwa ni majungu na kuwachonganisha wenzake, aliwaambia waandishi wa habari wambane Dk. Kitine awatajie jina lake, na akithubutu watashuhudia vita kati yao na kuongeza kuwa atamvisha taji la ‘Mzee wa majungu na uongo’.

“Naombeni waandishi mbaneni Kitine akitaja jina langu tu mtaona vita yake na mimi ambayo itakuwa kati yangu na Kitine sehemu ya pili na tutamvisha taji la mzee wa majungu na uongo,” alisema Membe.

Kadhalika, Membe alisema hawezi kukurupuka kusema kwamba atagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa kuwa bado hajasikia nafsi ikimsukuma kutoka moyoni kugombea nafasi hiyo.

Membe ambaye amekuwa akitajwa kuwa ana nia ya kugombea nafasi hiyo, alisema kuwa nafsi ikimsukuma ataweka wazi muda mwafaka utakapofika.

Waziri Membe alisema hayo jijini Dar es Salaam alipoulizwa swali hilo na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza msimamo wa Tanzania katika mgogoro wa Sahara Magharibi ambao unazihusisha Morocco na Sahara Magharibi.

Membe alisema anashangaa kusikia baadhi ya watu wakisema anajiandaa kugombea urais wakati bado nafsi yake haijamsukuma kufanya hivyo.

Waziri Membe alifafanua kuwa suala la kugombea urais siyo la kukurupuka na kwamba lazima mwenye nia hiyo awe na uwezo na kukidhi vigezo ili chama kimpitishe kama mgombea wa nafasi hiyo.

“Suala la kugombea urais siyo la kukurupuka, na mimi bado nafsi kutoka moyoni haijanisukuma kugombea, lakini wakati mwafaka ukifika na nafsi ikinisukuma nitaweka wazi kama nilivyoweka wazi kugombea nafasi ya ubunge baada ya nafsi kunisukuma,” alisema Membe ambaye ni Mbunge wa Mtama, mkoani Lindi.

NIPASHE lilimtafuta Dk. Kitine kuzungumzia madai ya Membe, ambapo alisema hana cha kusema na kwamba siyo lazima azungumzie kila jambo.

“Sina comment (cha kusema), kwani kila mtu anaweza kuwa na comment? Mimi sikumtaja mtu…sijui atapambana wapi,” alisema.

Dk. Kitine aliongeza kuwa: “Sina ugomvi na mtu yeyote.”

UKATA UBALOZINI


Akizungumzia taarifa kuwa ukata unasababisha baadhi ya mabalozi na maofisa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kuendelea kuishi nje licha ya kumaliza mikataba yao, alisema tatizo siyo fedha ila mabalozi hao wanajipanga kwa kuwa wengine wana watoto wanaosoma shule katika nchi hizo hivyo wanasubiri wamalize masomo ndipo warejee nchini.

Waziri Membe alisisitiza kuwa ofisi za ubalozi zimeshapelekewa fedha kwa ajili ya kugharimia mambo mbalimbali.

Akizungumzia msimamo wa Tanzania kuhusiana na mgogoro wa Sahara Magharibi, alisema Tanzania inaunga mkono wananchi wa Sahara Magharibi kupiga kura ya maoni ili kuamua kama wajitawale ama kubakia katika utawala wa Morocco.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles