Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tunapongeza waliofaulu vizuri kidato cha sita 2012

2nd May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Jana Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita wa mwaka 2012 yakionyesha kiwango cha kufaulu ni cha juu, yaani asilimia 87.58 sawa na watahiniwa 46,499 ya watahiniwa 53,255 waliofanya mtuhani huo.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa idadi ya waliofaulu haitofautiani sana mwaka jana ambayo matokeo yalionyesha kuwa waliofaulu walikuwa asilimia 87.24 sawa na wanafunzi 49,653.

Kama ambavyo imekuwa ikidhihirika katika miaka ya hivi karibuni, shule binafsi zimeendelea kufanya vizuri zaidi kuliko shule za serikali, hali inayoonyesha kuwa bado juhudi za serikali kuziwezesha shule za umma hazijazaa matunda ya kutosha.

Mathalan, katika wanafunzi bora watano wa mcheopuo wa sayansi, wanne wanatoka shule binafsi za Marian Girls wanafunzi wawili, Feza Boys’ wanafunzi wawili na mwanafunzi mmoja kutoka Minaki, ambayo ni shule ya serikali.

Hata hivyo, matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa katika kundi la shule bora kumi zenye wanafunzi zaidi ya 30, shule za serikali zimefanya vizuri kidogo kwa kutoa shule sita wakati za binafsi zikiingiza shule nne, wakati katika kundi la wanafunzi chini ya wanafunzi 30, hakuna hata shule moja ya serikali, inawezekana ni kwa sababu hakuna shule ya umma yenye wanafunzi wachache.

Kwa ujumla matokeo hayo yanaonyesha kuwa kiwango cha ufaulu kwa masomo ya sayansi ya fizikia, kemia, elimu viumbe na hisabati ni wa chini ikilinganishwa na masomo ya saana ya historia, lugha (Kiingereza na Kiswahili), Jiografia na yale ya biashara, uchumi na uhasibu.

Tunachukua fursa hii kupongeza wananfunzi na shule zao kwa ufaulu huu wa kutia moyo, tunawapongeza tukiamini kwamba wanatambua wajibu wao katika kuendeleza taifa hili katika nyanja za elimu ili kutoandoa katika janga linalotuandama la kuyumba kwa elimu yetu kwa muda mrefu sasa.

Tunazipongeza kwa njia ya kipekee shule zote za binafsi ambazo zimeendelea kung’ang’ania kileleni mwaka baada ya mwaka, lakini pia tunazipongeza kwa njia ya kipekee shule zote za umma ambazo nazo zimekataa kumezwa na wimbi na juhudi za shule binafsi na kuonyesha ushindani wa dhati katika kiwango cha ufaulu.

Tunaamini matokeo ya mwaka huu yana nafuu kubwa kwa sababu kiwango cha ufaulu kati ya darajala kwanza na la tatu kimeongezeka hadi asilimia 79.48 kutoka asilimia 79.41 mwaka jana.

Kiwango hili ni cha juu sana hasa kinapolinganishwa na hali ilivyokuwa kwa matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka jana kwani waliofaulu kati ya daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa ni takribani asilimia 10 tu.

Tunaamini kufaulu huku ni changamoto. Ni changamoto kwa sababu katika mazingira ya kawaida kwa kuwa waliovuka kidato cha nne na kujiunga na kidato cha tano ni wale waliofaulu vizuri ingelikuwa ni matarajio ya Watanzania kuwa walau kiwango cha kufaulu kingekuwa si chini ya asilimia 90.

Tunasema haya kwa kuwa tunaamini kwamba hakuna anayevuka mtihani wa kidato cha nne kwa bahati, ni matokeo ya juhudi na kujituma kwa bidii.

Kadhalika, tunachukua fursa hii kupongeza uamuzi wa Baraza wa kupunguza adhabu iliyotolewa kwa wanafunzi wa kidato cha nne wapatao 3,000 waliopatikana na udanganyifu na sasa adhabu yao imepunguzwa kutoka miaka mitatu hadi mwaka mmoja, tunaamini kuwa nafuu hii itatumiwa vizuri na wanafunzi hawa ili kujipanga upya kurejea darasani kwa sababu ni kweli tupu kwamba bila elimu vijana hawa hawatakuwa na lolote la maana maishani mwao.

Ni matarajio yetu kwamba hali iliyojidhihirisha mwaka huu kwa kupungua kwa kiwango cha udanganyifu katika mtihani huo kwa kuwa ni watahiniwa sita tu wamekamatwa, watatu wa shule na watatu wa kujitegemea, hali hii inaonyesha kuwa tatizo linazidi kupungua mwaka hadi mwaka.

Tungeomba Baraza lizidishe juhudi ili udanganyifu utoweke kabisa katika sekta ya elimu, hususan katika mitihani.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles