Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tujikite kutimiza fikra za Kanumba

14th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Ni wiki moja tangu kufariki kwa Steven Kanumba na siku nne tangu msanii huyo nguli wa filamu azikwe, lakini jamii kwa ujumla bado imeendelea kujikita katika siku ya kifo chake.

Wapo baadhi ya watu katika jamii ambao mpaka sasa wanakwenda kwenye kaburi la msanii huyo Kinondoni, Dar es Salaam kuhani baada ya wingi wa watu wakati wa mazishi yake kuwakosesha nafasi ya ama kumzika ama kutoa heshima za mwisho kwa mwili wake.

Wapo baadhi ya watu wabaya katika jamii ambao wameamua kutumia msiba huo wa msanii ambaye alidhihirika kuwa kipenzi cha maelfu ya wapenzi wa sanaa ya uigizaji kujinufaisha kiuchumi kwa kubuni miradi ya kuwaingizia fedha. Hawa walitengeneza fulana, CD za mazishi ama kutunga vitabu, chap chap.

Lakini, katika namna ambayo inaonyesha msiba wa Kanumba bado mbichi vichwani mwa wengi zaidi, mjadala wa hatma ya hatia ya kifo hicho ndiyo kwanza unashika kasi katika vyombo vya habari vya kawaida na mitandao ya kijamii ya ki-elektroniki.

Tulifarijika, Nipashe, mwanzoni mwa wiki baada ya baadhi ya wabunge kutumia fursa ya kikao cha mhimili huo wa dola kinachoendelea sasa mjini Dodoma kujaribu kuikumbusha jamii na serikali katika kufanya kile ambacho kitakuwa na manufaa kwa fani nzima ya uigizaji na jamii ya nchi yetu kwa ujumla, kama ambavyo zilikuwa ndoto za marehemu.

Mijadala kama kifo cha Kanumba ni mauaji ama la, kilikusudiwa ama la, kilisababishwa ama la, mtuhumiwa 'Lulu' ni mtu mzima ama mtoto, ni masuala ya kisheria ambayo kwa bahati nzuri yanaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (ya jinai).

Aidha pameibuka mjadala mwingine kama hatma ya 'Lulu' ambaye bado ni mtuhumiwa tu ni sakata la kijinsia ama la kiharakati. Na mingine kama hiyo ambayo haina maana kuendelezwa, Nipashe tunaona.

Haina maana kuendelezwa, tunaona, kwasababu maisha ya marehemu Kanumba yameacha kishindo kikubwa katika ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Maisha mafupi ya marehemu Kanumba yametukumbusha Watanzania kuwa penye nia pana njia na ndiyo maana msanii huyo, kwa kujiajiri mwenyewe, akafanikiwa kuwa na maisha ambayo yanaweza kuonewa wivu wa kimaendeleo na vijana wengi; hata wenye ajira.

Aidha, maisha ya Kanumba yalimuwezesha kuwa na kampuni iliyokuwa si tu ikitoa ajira kwa vijana bali pia iliyokuwa na kila dalili ya kuinua vipaji vingi mno vichanga vya ugizaji nchini.

Hapa ndipo tunapojiuliza, ni wangapi wangepita katika mikono ya Kanumba kama angeishi angalau muda stahiki ambao umetajwa katika vitabu vya dini?

Lakini maisha ya Kanumba pia yametufundisha kuwa na moyo wa kuisadia jamii, kila mmoja kwa nafasi yake na kwamba hilo linawezekana.

Na mipango yake ya kujenga shule kwa ajili ya kukomboa eneo la Mpiji mkoani Pwani kielimu, kwa mfano, inathibitisha hilo.
Ni rahisi kutoyaona hayo, ama kuyasahau haraka, kama jamii itaendelea kujikita katika siku ya Aprili 7.

Hivyo badala ya jamii kuendelea kujadili hatia, umri, uadilifu wa wanasiasa na wanaharakati na vingine kama hivyo, tutafakari kifo cha Kanumba kwa mapana yake na kwa pamoja na serikali, tuhakikishe kuwa fani ya uigizaji filamu inakomboa wasanii na kuiendeleza jamii kama ambavyo marehemu aliamini.

Kuna mengi ya vijana kufanya wakati huu wakitafakari maisha ya Kanumba kuona jinsi ambavyo wanaweza kufuata nyayo zake kwa manufaa yao na ya taifa lao kwa ujumla.

Nafasi hiyo itapatikana wapi kama jamii haijashituka kuwa wakati ni huu na unaitupa mkono?

Kuna mengi yaliahidiwa na viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wakati wa maombolezo ya msiba wa Kanumba na kwenye mazishi yake.

Jamii itayakumbuka hayo na kudai yatimizwe kama mpaka leo bado imejikita katika tukio lenyewe la kupotea kwa uhai wa Kanumba?

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles