Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba yapaa, Yanga `ndembendembe`

16th April 2012
Print
Comments
Kikosi cha Simba

Goli lililofungwa na kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Patrick Mafisango, liliipeleka Simba karibu na ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati mahasimu wao wa jadi, Yanga, wakipoteza matumaini ya kutetea ubingwa msimu huu baada ya kukubali kipigo kisichotarajiwa cha mabao 3-2 kutoka kwa 'ndugu' zao Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana.

Matokeo hayo yaliifanya Simba izidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi na kukaribia ubingwa walioupoteza kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kufikisha pointi 53 na kubakiza mechi tatu, pointi tatu zaidi ya Azam inayowafuatia katika nafasi ya pili.

Yanga ambayo hivi karibuni ilipata pigo baada ya kunyangang'anywa pointi tatu walizopata katika ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Coastal Union kwa kumchezesha Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa akitumikia adhabu, sasa watasubiri muujiza ili kutetea ubingwa. Wanakamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi 43 na kubakiza mechi nne kabla ya msimu kumalizika.

Mafisango aliifungia Simba bao pekee la ushindi kwa shuti kali la karibu na lango wakati zikiwa zimebaki dakika 10 kabla ya mechi kumalizika, akimalizia vyema krosi safi kutoka kwa Haruna Moshi 'Boban'.

Awali, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kusababisha kosakosa kadhaa, zikiwemo za dakika ya 21 wakati Gervais Kago na Boban walipojikuta wakianguka na kuikosesha Simba goli la utangulizi kufuatia krosi nzuri iliyotoka kwa kwa Emmanuel Okwi.

Ruvu walikosa bao la wazi katika dakika ya 48 wakati Abdallah Juma alipopiga shuti lililotoka nje ya lango tupu wakati kipa Juma Kaseja akiwa ameshatoka.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovik alisema kuwa amefurahishwa na ushindi walioupata, licha ya kukiri kwamba mechi ilikuwa ngumu kuliko walivyotarajia.

KICHAPO YANGA
Siku mbaya kwa Yanga ilionekana mapema jana wakati walipojikuta wakipelekeshwa kwa gonga safi za wenyeji na kutanguliwa kwa mabao matatu kabla hata ya mapumziko.

Totowaliwastua 'kaka' kwa kufunga bao la utangulizi katika dakika ya 18 kupitia kwa Mussa Said, ambaye alipiga shuti kali baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Kamna Salum.

Dakika sita baadaye, Iddy Mobby aliiandikia Toto bao la pili kwa kuunganisha vyema mpira wa adhabu ndogo kutoka wingi ya kulia.

Said aliwaliza tena Yanga katika dakika ya 39 baada ya kugongeana pasi safi na Mohamed Soud kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa Shaaban Kado wa Yanga.

'Wanajangwani' walicharuka na kupata bao la kwanza wakati zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya mapumziko baada ya Mganda Hamis Kiiza kutumia vyema krosi ya Mzambia Davis Mwape.

Katika dakika ya 65, kiungo wa kimataifa wa Yanga, Mrwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas' alifanya kazi nzuri na kutoa pasi iliyounganishwa wavuni kwa kisigino na Kiiza.

Yanga waliopania kusawazisha walifanya mashambulizi kadhaa lakini mabeki wa Toto, wakiongozwa na Mobby, walisimama imara na kuondosha hatari zote, hivyo mabingwa watetezi wakajikuta wakipata kipigo chao cha nne msimu huu.

Ushindi huo uliipandisha Toto kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi ambapo sasa inakamata nafasi ya 10 baada ya kufikisha pointi 23 na kubakiza mechi nne kabla msimu kumalizika.

Katika mechi nyingine ya Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, wenyeji Villa Squad waliendelea vyema na kampeni yao ya kujinasua kutoka kwenye ukanda wa kuteremka daraja baada kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Villa wamefikisha pointi 22 na sasa wanakamata nafasi ya 11,  lakini wakibakiwa na mechi tatu tu wakati African Lyon wanaowafuatia kwa tofauti ya pointi moja huku wakiwa na mechi moja zaidi ya kiporo.

Vikosi
Yanga: Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Abou Ubwa/Kenneth Asamoah (dk. 44), Chacha Marwa, Athumani Iddi 'Chuji', Godfrey Bonny, Rashid Gumbo, Haruna Niyonzima, Davis Mwape, Hamis Kiiza na Kigi Makassy.

Toto: Erick Ngwengwe,Idd Mobby, Erick Magesa, Peter Mutabuzi, Ladislaus Mbogo, Tete Kanganga, Emmanuel Swita, Mohamed Soud, Enyina Darlington, Kamana Salum na Mussa Said.

Imeandikwa na George Ramadhani, Mwanza na Somoe Ng'itu, Dar es Salaam.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles