Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbunge wa CCM awasuta Viongozi

21st May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari

Mbunge wa Mwibara (CCM), Wilayani Bunda, Kangi Lugola, ametema cheche kwa kuwaomba wachungaji wilayani Arumeru mkoani Arusha kufanya maombi kwa viongozi walioko madarakani, ili waweze kuachana na rushwa inayoangamiza taifa na kusababisha kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Alisema hayo jana wakati wa ibada ya shukrani iliyoandaliwa na Kanisa la FPCT Kilinga kwa ajili ya kumuombea Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari kumwepusha na majaribu mbalimbali baada ya kushinda ubunge.

Lugola alisema ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuna kikundi cha watu wachache wenye kutanguliza matumbo mbele  na kusahahu mpango wa Mungu wa kuleta ukombozi wa wananchi.

“Mimi pamoja na kwamba nipo ndani ya CCM lakini kwa kuwa nimeokoka na nampenda Mungu, nachukia ufisadi na watu hawa na ndio sababu niko mstari wa mbele kupambana na mafisadi,” alisema Lugola.

Lugola alikuwa miongoni mwa wabunge wa CCM walioweka saini ya kutaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda ang’oke kufuatia mawaziri sita kutajwa kwa ufisadi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kauli mbiu ya maisha bora kwa kila Mtanzania ingefanikiwa na kuwezekana pale viongozi walioko madarakani watakapoacha
rushwa, vinginevyo hakuna kitu.

Lugola alisema kuwa Tanzania sio nchi maskini bali wananchi wake ndio maskini, hivyo wanahitaji wachungaji waungane pamoja kuombea viongozi wa Serikali na baadhi ya wabunge waliojitoa kimasomaso kupiga vita ufisadi bila kujali vyama vyao.

“Naomba jamani mtuombee na hawa viongozi wetu serikalini ombeeni kwa nguvu sababu rushwa imeharibu nchi hii, rasilimali zetu zinaliwa tu na wachache,” alisisistiza.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, alisema kuwa wengi wa wabunge wameingia bungeni kwa kutumia rushwa na ndio sababu wapo mstari wa mbele kuwapiga vita wabunge wanaopinga ufisadi hivyo wanahitaji neema ya Mungu.

Awali katika misa ya shukrani Watanzania wametakiwa kuepuka kuchagua viongozi wanaotumia rushwa katika chaguzi, ambao wakishinda wanatumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao wenyewe.

Akihubiri kwenye ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la FPCT Kilinga, Langael Kaaya, alisema lilipofika kwa sasa, linalazimika kupata viongozi wasio na mapenzi na wananchi kwa sababu ya rushwa.

“Tunahitaji kuomba sana kila mmoja aombe, ili tuweze kuepukana na tatizo hili la rushwa , tuchague viongozi walio na mapenzi ya kweli kwa wananchi,” alisema Mchungaji Kaaya.

Mchungaji Kaaya alisema rushwa inatumika kuharibu na kupoteza haki, pamoja na kuharibu mipango ya Mungu, hata pale wananchi wanapohitaji kufanya mabadiliko, hayafanyiki na yanavurugwa na rushwa.

Aidha aliomba watu kufunga na kukataa dhambi ya mauaji, inayofanywa na baadhi ya watu katika eneo la Meru ya kuuwa watu kwa kuchinja na kuwanyonga hasa baada ya kumalizika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki ili Mungu awasamehe kwa dhambi hiyo.

Alisema uchaguzi umeisha na sasa kilichopo ni kufanya kazi za wananchi na hivyo yuko mstari wa mbele, kushirikiana na Madiwani wa CCM katika kuleta maendeleo na kuona kwamba watakaokwamisha jitihada hizo watashughulikiwa.

Nassari alisema ana kila sababu ya kumshukuru Mungu, kabla ya kwenda kutembelea wananchi katika kila kata kuwashukuru kama wanavyomwomba, ili kujiweka karibu zaidi na Mungu, ameamua kuanza kutoa sadaka kanisani kwanza.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles