


.jpg)
Askari polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, amejeruhiwa na kukimbizwa hospitali baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kuanguka wakati akiongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete.
Msafara huo wa Rais Kikwete, ulikuwa ukitokea Ikulu kwenda msibani eneo la Kimara, jijini Dar es Salaam jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea ajali hiyo na kumtaja askari aliyejeruhiwa kuwa ni D.7380 Sajenti Steven Raphael Laizer.
“Ni kweli amejeruhiwa. Aliteleza wakati anaongoza msafara wa Rais,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Rombo, Ubungo, jijini Dar es Salaam, baada ya pikipiki hiyo kuteleza na kuanguka.
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Kenyela alisema askari huyo aliteguka bega na kupata michubuko sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema kufuatia ajali hiyo, askari huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.
Hata hivyo, Afisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesha, hakupatikana jana kuelezea hali ya askari huyo.
Kamanda Kenyela alisema pikipiki hiyo iliteleza kutokana na utelezi uliotokana na majimaji yaliyokuwa barabarani kabla ya kwenda kuparamia tuta na kupoteza mwelekeo na kuanguka.
Alisema majimaji hayo yalitokana na mvua iliyonyesha katika eneo hilo jana mchana.
“Mvua ilikuwa inanyesha. Mbele kulikuwa na majimaji. Kulikuwa na tuta. Tunafikiri ndilo lililomtoa kwenye mfumo wa uendeshaji wa pikipiki,” alisema Kamanda Kenyela.
Aliongeza: “Amechubuka sehemu mbalimbali za mwili wake na bega lake limeteguka.”
Hata hivyo, Kamanda Kenyela alisema hali ya askari huyo inaendelea vizuri na kwamba, ajali iliyotokea ilikuwa ni ya kawaida na ya bahati mbaya.