Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mafao miaka 55: Wabunge waache `kujishaua`, serikali isikilize kilio cha wafanyakazi

29th July 2012
Print
Comments

Kila kona ya nchi hivi sasa ni kilio cha wafanyakazi tangu kutangazwa kuanza kwa utekelezaji wa mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012, ambayo yanawazuia kuchukua fedha zao zilizohifadhiwa katika mifuko hiyo (NSSF na PPF) mpaka watimize miaka 55 au 60.

Kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria hiyo, ambayo Rais Jakaya Kikwete ameshaweka saini kuwa sheria, wafanyakazi wa sekta zote hawatapewa mafao yao kama wakiacha kazi mpaka watimize miaka 55 ya kustaafu kwa hiari au miaka 60 ya kustaafu kwa lazima au wapate ulemavu wa kudumu. Miongoni mwa waliojitokeza hadharani kupinga sheria hiyo, ni Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, ambaye alikaririwa akisema sheria hiyo ni wizi wa fedha za wafanyakazi.

Pia Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyinginezo (TAMICO) Wilaya ya Geita, Benjamin Dotto, alisema wanapinga sheria hiyo kwa sababu ni ya kibaguzi na inapingana na Katiba ya nchi, ambayo inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria.

Aidha, wafanyakazi 600 wa migodi saba ya dhahabu iliyopo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tabora, wameripotiwa kuacha kazi na wengine 4,000 kuwasilisha barua kwa waajiri wao za kusudio la kuacha kazi kupinga sheria hiyo.

Kwa uchache, kilio hicho cha wafanyakazi kinaashiria kwamba, sheria hiyo haikubaliki. Sababu inapora uhuru na haki ya mfanyakazi kujiendeleza au kuendesha maisha yake iwapo ajira yake itasitishwa kwa namna yoyote kabla hajatimiza umri huo.

Pia hakuna anayejua ni wafanyakazi wangapi wataifikia miaka 55 na kunufaikia na mafao yao yanayotokana na jasho lao.

Vilevile, hakuna anayejua kiasi atakachopata mfanyakazi iwapo atabahatika kufikisha umri huo. Hiyo ni kutokana na shilingi ya Tanzania kuporomoka na mfumuko wa bei kuongezeka kila uchao.

Zipo sababu nyingi za msingi zinazoshawishi sheria hiyo isikubalike. Mojawapo, ni kufichwa katika sheria hiyo kipengele kinachowanyima wafanyakazi uhuru na haki ya kuchukua mafao yao katika muda wanaoutaka. Hili halikuwekwa wazi wakati mchakato wa kujadili na kupitisha mabadiliko ya sheria hiyo ukifanyika. Badala yake, kilichofanyika kama inavyosemwa mitaani, wafanyakazi ‘walipigwa changa la macho’ kwanza ndiyo sheria hiyo ikapitishwa! Kwa ufupi, hakukuwa na uwazi wowote katika mchakato huo. Mabadiliko ya sheria hiyo hayakusikika kama inavyofahamika yakipelekwa kwenye kamati za Bunge kujadiliwa.

Kwa jumla, hakukuwa na ushirikishwaji sahihi na kamilifu kwa wadau, vikiwamo vyombo vya habari katika mchakato mzima hadi Bunge likapitisha sheria hiyo.

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) ilidai katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Alhamisi wiki hii kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo ulihusisha wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, Chama cha Waajiri (ATE) na serikali. Hoja hapa si kuhusisha watu hao tu. Bali kuwahusisha kiusahihi na kikamilifu, aina gani ya watu waliohusishwa, namna gani walihusishwa na waliwezeshwaje kuelewa sheria hiyo. Na si vinginevyo.

Hatua ya wafanyakazi kupinga sheria hiyo ni ishara kwamba, mambo hayo hayakuzingatiwa wakati wa mchakato huo. Kitendo cha Bunge, ambalo pamoja na kujua sheria hiyo kwamba, inapora uhuru na haki ya mfanyakazi, limeipitisha, sioni sababu ya kutoamini kauli ya Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola, na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kwamba limekosa umakini na ni zembe!

Tukitafakari hilo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama, ameahidi bungeni kwamba, atawasiliana na Spika wa Bunge, kuitisha Kamati ya Uongozi wa Bunge kujadili sheria hiyo. Kauli hiyo ya Mhagama ilifuatia ushauri uliotolewa na Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo, kutaka malalamiko ya wafanyakazi na mabadiliko ya sheria hiyo yajadiliwe na Bunge na kuungwa mkono na wabunge wengi bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Pia wabunge; Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) na Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema), walitilia mkazo kutaka suala hilo lijadiliwe na Bunge.

Binafsi, sioni uhalali wa Bunge kuijadili sheria hiyo. Kwani ni Bunge kuzidi kujidhalilisha tu. Kitendo cha kuipitisha sheria hiyo tayari kimeshawavua nguo wabunge. Wako uchi! Inashangaza! Badala ya kuingia uvunguni ili wajisitiri, wao wanapanda juu ya meza! Kwa hili wabunge hawana cha kujitetea. Wameshaharibu. Wakae kimya. Waache ‘kujishaua’. Wasubiri hadi hapo labda serikali itakapopeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria hiyo. Wajadili muswada huo. Na si vinginevyo!

Sina kumbukumbu sahihi kama Jafo, Zitto na Lissu walikuwapo bungeni wakati mabadiliko ya sheria hiyo yalipopitishwa na Bunge au la. Kama hawakuwapo, sikumbuki kama kutokuwapo kwao kulitokana na udhuru wa kimsingi au utoro bungeni au la.

Lakini inavyoonekana hadi sheria hiyo inapitishwa na Bunge, baadhi ya wabunge hawakuwa bungeni. Walikuwa wanaendelea na biashara zao. Hao ni wale, ambao Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivi karibuni alishindwa kuendelea kuwavumilia. Akawaonya dhidi ya tabia yao mbaya ya utoro bungeni.

Yawezekana wabunge wengine wakati sheria hiyo inapitishwa walikuwa wakisinzia bungeni. Na wale walioipitisha hakuna ubishi hawakuwa makini.

Sababu nyingine ni vyama vya wafanyakazi, ambavyo siku zote vinatarajiwa kuwa watetezi wa wafanyakazi. Kama kweli vilishirikishwa katika mchakato unaoelezwa na SSRA halafu sheria hiyo ikapitishwa, navyo pia haviko makini.

Na ndio maana wanaoonekana kulalamikia mabadiliko ya sheria hiyo ni wafanyakazi. Hawaitaki sheria hiyo. Wanataka wawe huru. Isiwepo sheria inayowanyima uhuru na haki ya kuchukua hela zao wanapozitaka.

Sababu zote iliyotolewa na SSRA kutetea sheria hiyo kwamba, ni kuhakikisha mwanachama anapostaafu, anapata mafao bora kumudu maisha uzeeni, haikubaliki.

Wafanyakazi ni watu wazima. Wanajua kustaafu kwao. Hivyo, hawawezi kupangiwa kustaafu kwao.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona serikali inasikiliza kilio cha wafanyakazi. Ichukue hatua ya kupeleka haraka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria hiyo ili kurejesha uhuru na haki ya wafanyakazi ya kuchukua hela zao katika muda wanaoutaka. Siku zote serikali ya watu huwasikiliza watu.

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. Baruapepe: muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment