Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mke wangu anachat na wanaume, nakonda sijui nichukue hatua gani!

13th May 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, meseji za kwenye simu za viganjani bado zinazidi kutesa ndoa. Wapo wasomaji wetu mbalimbali ambao wameshaleta malalamiko yao wakitaka ushauri nini cha kufanya.

Wapo waliodiriki kusema wanazihama nyumba zao kutokana na kero hiyo, na zaidi pale tabia hiyo ya wake zao kuchat kuendelea hata baada ya kuonywa.

Kabla sijaendelea msomaji wangu, hebu msikie mwenzetu huyu ambaye mkewe anampelekesha vilivyo, lakini bado anatafakari afanye nini huku akitegemea sana ushauri toka kwa wasomaji wengine. Alituma meseji kadhaa kuelezea tatizo lake kama ambavyo itasomeka hapa chini.

“Aunty, mke mwema huyu kaanza kubadilika 2010. Anafanya biashara ya kuuza vipodozi kwenye mabasi ya mikoani. Kwenye hayo mabasi wanatozwa pesa kidogo kwa ajili ya safari zao fupi fupi.

Angalia rushwa ya ngono na mada yako uliyowahi kuandika kuhusu ujumbe wa simu za viganjani zinavyoharibu ndoa.

Akapata mabwana wawili madereva(simu zao nahifadhi kwa sasa), maudhi ndiyo usipime yakaanza kufumuka.

Penzi likamkolea kwa dereva wa basi. Wakaanza kuchati hata nikiwa naye kwenye sita kwa sita. Nikaona siyo kweli, akawa mpumbavu pacha wangu, hafuti SMS(meseji) hata zikiwa 100.

Akiwa anakoroma kwa usingizi, nachukua simu yake naifungua, nilitaka kumuua siku hiyo. Poa sikufanya hivyo. No anami Aunt nikatafuta suluhu kwa ndugu na jamaa hasa upande wao. Ajabu akagoma kabisa eti hana mahusiano naye.

Nikawaambia wanawake anaofanya kazi nao, wakamkanya, alikiri shetani alimpitia. Baada ya hapo simu yake akawa anaificha kama bangi.

Lakini poa, nikampigia mtu wake (buzi lake) tukaongea kistaarabu sana, akaniambia nadhalilishwa na mke wangu, aibu.

Nikawa naendelea kumsihi mtu wake kwamba aachane na mke wangu kwani hakuna amani hata kidogo. Mmoja wa hao mabwana zake akanipigia simu akiniambia wapi tuonane tuweke mambo sawa hata sikutekeleza.

Mara nyingi huwa natumia hivi, anaficha simu kila tunapoingia kitandani. Usiku mwingi naitafuta naipata nawasha nafungua meseji, nakuta wanaendelea kuchati. Hapa inaonyesha mke wangu huwa anamwambia mumewe kuwa asiogope hakuna kitakachomtokea mtu wake Kati ya meseji za mke wangu kwa mtu wake huwa anamwita mume ilhali mama watoto akijua kabisa kuwa tulifunga ndoa halali Kanisa Katoliki Ukonga.

Mwanamama huyu huwa nampigia simu anikute sehemu kwa chakula hasa jioni anapokuwa anarudi kwenye mihangaiko nay eye wakati mwingine huwa ananiuliza niko wapi labda kama kwenye saa tatu hivi usiku. Sijawahi kukataa wala yeye hakatai pale ninapomuelekeza aje. Na mara nyingi tunapenda sehemu hiyo hiyo, akinialika yeye au mimi nimuite yeye.

Mwezi uliopita mwenetu binti alirudi toka likizo ya shule. Anasoma bweni mkoa wa Pwani. Alikuwa anajiandaa kuondoka. Na kipindi hicho chote nimekuwa mpole sana kwa heshima ya mtoto wetu mpendwa Baada ya mwaka mzima bila mapenzi kunako sita kwa sita.

Hata pale anapokubali inabidi niingie uwanjani na soksi kubwa kwani ni ugomvi mkubwa kwanini natumia soksi. Anti usipime bali acha tu, ananisumbua hadi nakonda, sili vizuri nawaza, nakonda.

Wiki mbili wakati tunamsukuma mtoto kwenda shule, nilipitia tena simu yake mara mbili hivi sijaona meseji na maharunanga zake wala za mke wangu kwenda kwa mumewe. Ngoja nichungulie tena nione, lakini cha kufanya nimkimbie au nimsubirie? Niambie aunt”, anamaliza ujumbe wake wa mwisho.

Mpenzi msomaji, bila shaka umemsikia vema ndugu yetu huyu kwa masahibu yanayomkuta kila kukicha. Anasema hata kukonda amekonda kwa kufikiria visa vya mkewe.

Jamaa huyu inaonekana anampenda sana mkewe na ndiyo maana angali anavuta kasi kuchunguza nyendo zake kwa kuwa haamini kinachotokea.

Anafikia hatua hata ya kuzungumza na wanaume wanaovunja ndoa yake akitaka kujua kulikoni. Na kibaya zaidi anaambulia kuambia na mmoja wa mabwana hao kwamba mkewe anamdhalilisha.

Mpenzi msomaji, usione watu wanatembea barabarani ukadhani akili zao ziko sawa. Ziko mguu upande kabisa kutokana na suluba wanazokumbana nazo huko majumbani mwao. Kama siyo mama msumbufu, basi ni baba au watoto. Maisha Ndivyo Yalivyo. Au siyo msomaji wangu?

Naam. Tatizo kubwa hapa ni kwamba mke ndiyo tatizo ndani ya ndoa hii. Siyo mwaninifu kabisa na ushahidi ni meseji ambazo mumewe amekuwa akizinasa kwenye simu yake. Na isitoshe hata alipobanwa bibie huyu alikiri kuchat na wanaume nje ya ndoa.

Jamaa huyu, hata hivyo anaweza kujipa muda kuona kama mke huyu atajirekebisha. Lakini akishindwa, basi arudi kwa washenga, kikao cha wazee wa pande zote na huko ikishindikana aombe talaka mahakamani kila mtu ahangaike kivyake.

Katika maandiko ndani ya Biblia Takatifu kitabu cha Methali sura ya 25 mstari wa 24 una maneno yanayosomeka hivi; “Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani pamoja na mwanamke mgomvi”. Hayo ni maneno ya Mungu mwenyewe.

Mpenzi msomaji, kwa leo niachie hapa ili nikupe fursa nawe uchangie kwa kumpa ushauri, maoni ndugu yetu huyu kwa msukosuko alio nao.

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; [email protected]

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles