Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba yaaga kishujaa Afrika

14th May 2012
Print
Comments
Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, Simba

Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, Simba, waliaga michuano hiyo baada ya kutolewa na Al Ahly Shandy kwa penalti 9-8 kufuatia kichapo cha magoli 3-0 katika mechi yao ya marudiano kwenye Uwanja wa Shandy jana usiku.

Katika hatua ya 'matuta' ambapo kila timu ilipiga penalti 10, wachezaji wawili wa Simba Patrick Mafisango na kipa Juma Kaseja walikosa na Wasudan wakakosa moja na kuhitimisha ulioonekana kuwa msimu mzuri kwa Simba, ambao ndio kwanza wametoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Simba ambayo ilishinda 3-0 katika mechi yao ya awali na kucheza vyema katika kipindi cha kwanza jana kilichomalizika kwa matokeo ya 0-0, walionekana kama vile wanakaribia kusonga mbele, lakini kukosekana kwa umakini katika safu ya ulinzi wa kati iliyoundwa na veterani Victor Costa na Kelvin Yondani, kuliwapa wenyeji goli la kuongoza sekunde chache tangu kipindi cha pili kuanza.

Farid Mohammed aliipatia Shandy bao la kwanza katika dakika 46 kufuatia shambulizi la moja kwa moja kutokea katikati ya uwanja na mabeki kushindwa kumdhibiti mfungaji aliyepita katikati yao.

Wenyeji walipata goli la pili katika dakika ya 50 lililofungwa kwa kichwa kutokana na mpira wa 'fri-kiki' ya nje ya boksi na udhaifu wa Simba katika kudhibiti mipira ya 'fri-kiki' almanusura iwape Shandy goli la tatu katika dakika ya 58 kutokana na mpira wa adhabu ndogo lakini kichwa cha mchezaji wa Shandy kiligonga 'besela' wakati kipa Juma Kaseja akiwa ameshakubali matokeo.

Farid Mohammed alifunga goli la tatu kwa Shandy na la pili kwake usiku wa jana katika dakika ya 60 baada ya mabeki wa Simba kushindwa kudhibiti 'presha' ya wenyeji langoni mwao na kufanya mechi kumalizika kwa matokeo ya 3-0, sawa na waliyopata Simba wiki mbili zilizopita katika mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam. Mechi moja kwa moja iliingia katika hatua ya kupigiana matuta bila ya dakika 30 za nyongeza. 

Katika penalti 5 za kwanza kila timu ilikosa moja huku Mafisango akikosa kwa upande wa Simba wakati aliopata walikuwa ni Felix Sunzu, Machaku salum, Emmanuel Okwi na Shomary Kapombe.

Wakati wa kupigiana penalti moja-moja, wachezaji wa Simba waliofunga bila ya kukosa walikuwa Kelvin Yondani, Victor Costa, Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah hadi penalti ya kumi ambayo Kaseja alikosa baada ya yeye kufungwa na kipa mwenzake wa Shandy. 

Simba walicheza vyema katika kipindi cha kwanza na wangeweza kupata bao katika dakika ya 34 wakati Uhuru Selemani alipopiga shuti kali kutokea nje ya boksi ambalo lilipanguliwa na kipa wa Shandy kabla ya kugonga besela na kuwa kona.

Mabeki wa Shandy walishindwa kuikoa vyema kona hiyo na kumpa nafasi kiungo Patrick Mafisango kupiga shuti la jirani na nguzo ambalo hata hivyo lilipanguliwa na kipa wa wenyeji na kuwa kona nyingine ambayo haikuzaa matunda.

Kikosi cha Simba kilikuwa: Juma Kaseja, Shomary Kapombe, Amir Maftah, Kelvin Yondani, Victor Costa, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Uhuru Selemani/ Salum Machaku (dk.22), Emmanuel Okwi, Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles