Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Bavicha Arusha wamng`ang`ania Shibuda

22nd May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda

Baraza la Vijana Chadema Mkoa wa Arusha (Bavicha), inaunga mkono tamko la uongozi wake wa Taifa la kulaani hatua ya mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, kutoa tamko la kukidhalilisha chama, mbele ya viongozi wa CCM na kumfananisha na uhaini ndani ya chama.

Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro, alisema kimsingi baraza hilo halina tatizo na nia ya Shibuda kugombea Urais, bali kauli yake aliyoitoa kuwa chama pekee kinachoweza kushika dola ni CCM, hivyo wanalaani kauli hiyo.
Alisema Chadema imejipanga kuchukua dola, sababu ina mfumo mzuri wa kiuongozi kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.

Alisema Shibuda anaweza kuwa anatumiwa na CCM kuvuruga mipango ya Chadema, kutokana na operesheni ‘Vua Gamba, Vaa Gwanda, ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuvuna maelfu ya viongozi wa CCM wanaohamia Chadema.

Nanyaro alisema mkakati unaotumiwa na Shibuda, hautavuruga ndoto na mipango ya Chadema na kwamba chama hicho kimepitia changamoto nyingi lakini kilifanikiwa kuvuka salama.

Alisema Chadema kimewahi kuchukua maamuzi magumu kwa kuwafukuza baadhi ya madiwani wake mkoani Arusha na bado kikabaki imara “katika hili la Shibuda wanaomba chama kichukue maamuzi magumu, hata kwa gharama ya jimbo.”

“Ukiwa na askari katika kikosi chako ambaye anaamini majeshi ya adui ni bora zaidi na yanastahili kushinda vita, askari huyo anakuwa ni msaliti na anapofanya kazi au jitihada ya kutaka adui ashinde, kijeshi huo ni uhaini, hivyo  Shibuda kutangaza kuwa anataka kugombea Urais kupitia Chadema mwaka 2015 siyo tatizo, tatizo ni kukidhalilisha chama mbele ya CCM,” alisema.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles