Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

BFT yashindwa kuandaa ngumi Afrika

7th July 2012
Print
Comments
katibu wa BFT Makore Mashaga

Shirikisho la ngumi za ridhaa (BFT) limeshindwa kuandaa mashindano ya wazi ya ngumi ya nchi za Afrika kutokana na kukosa ukumbi wenye hadhi ya kuandaa mashindano ya kimataifa.

Michuano hiyo inayotambulika na Shirikisho la mchezo huo duniani (AIBA) ilipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na NIPASHE, katibu wa BFT Makore Mashaga alisema Tanzania ilipewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo katika mkutano mkuu wa nchi za Afrika uliofanyika April nchini Morroco, wakati wa michuano ya ngumi ya kutafuta nafasi ya kushiriki michezo ya Olimpiki.

"BFT tulipewa nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano hiyo, lakini tumeshindwa kutokana na kutokuwa na ukumbi wenye ulingo wa viwango vya kimataifa," alisema Mashaga.

Alisema kutokana na hilo, tayari wameliandikia barua Shirikisho hilo, ya kuwa hawawezi kuandaa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Hata hivyo Mashaga alisema kutokana na wao kushindwa kuwa wenyeji wa michuano hiyo, bado timu ya taifa ya ngumi inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujianda kushiriki katika mashindano hayo.

"Timu ya taifa bado inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo," alisema Mashaga.

Alisema endapo AIBA itatoa uwenyeji kwa kwa nchi nyingine, timu ya taifa ya ngumi itakwenda kuliwakilisha taifa kwenye michuano hiyo.

Wakati huo huo, mashindano ya taifa ya ngumi yamepangwa kufanyika Agosti 25 hadi 31 katika Uwanja wa Ndani wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Mashaga alisema michuano hiyo inatarajia kushirikisha mabondia kutoka mikoa yote hapa nchini.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment