Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tanzania yaisambaratisha Lesotho netiboli Afrika

9th May 2012
Print
Comments
Nyota wa timu ya netiboli ya tanzania (Taifa Queen), Mwanaidi Hassan (kulia) akijaribu kumdhibiti mchezaji wa timu wa timu ya Lesotho, Momojaki Tjabane, wakati wa mechi yao ya uchunguzi wa michuano ya ubingwa wa Afrika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu ya taifa ya netiboli ya Tanzania, Taifa Queens, ilianza kwa kishindo michuano ya ubingwa wa mchezo huo Afrika baada ya kuipa kipigo cha "paka-dokozi" timu ya taifa ya Lesotho cha 57-13 katika mechi ya ufunguzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mshindi wa zawadi ya gari ya Mwanamichezo Bora wa TASWA wa Mwaka jana, Mwanaidi Hassan ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo wa jana baada ya kufunga magoli 38, huku Pili Peter akiongeza 17 na Irene Elias akifunga mawili.

Taifa Queens ilitawala mchezo tangu mwanzo na hadi robo ya kwanza ilipomalizika wenyeji wa michuano walikuwa mbele kwa magoli 13-3 na wakati wakienda mapumziko Tanzania walikuwa mbele kwa magoli 23-9.
Robo ya tatu ilipomalizika, Tanzania walikuwa mbele kwa magoli 40-13 na ndipo Mwanaidi alipopumzishwa akiwa tayari amefunga magoli 38 na nafasi yake kuingia Pili, aliyemalizia robo ya nne na kufunga magoli 17.

Nahodha wa Taifa Queens, Lilian Sylidion, alisema ushindi wao umetokana na hamasa kubwa waliyoipata wachezaji kutokana na michango ya Watanzania kupitia kamati ya maandalizi pamoja na mazoezi ya kila siku chini ya makocha wao.

Michuano hiyo ya siku tano, itaendelea tena leo asubuhi ambapo Malawi watawakabili Zambia, Uganda watawavaa Botswana na Zimbabwe watacheza dhidi ya Lesotho.

Katika mechi za mchana leo, wenyeji Tanzania watashuka uwanjani kuwakabili Malawi, Zambia tena watacheza na Botswana, huku Uganda ikiwakabili Zimbabwe.

Timu ya Namibia imeshindwa kuja kutokana na kukosa fedha.

Wakati wa sherehe ya ufunguzi wa michuano hiyo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alilitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuvifuatilia kwa karibu vyama vya michezo vinavyoandaa michuano au timu za taifa zinazoenda kuliwakilisha taifa nje ya nchi ili kuliepushia taifa aibu kutokana na maandalizi ya zimamoto.

Alisema kutokana na kutokana na udhaifu katika uwajibikaji wa baadhi ya viongozi, vyama vimekuwa vikikimbizana katika dakika za mwisho kabla ya michuano kuanza jambo ambalo linachangia kutofanya vizuri kwa wanamchezo wetu kitaifa na kimataifa.

Alisema kuanza maandalizi mapema kunasaidia na kwamba hicho ndicho kilichowasaidia CHANETA, chama cha netiboli Tanzania, kufanikisha kuandaa michuano hiyo ya Afrika.

Naye mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, mama Tunu Pinda, ambaye ni mke wa waziri mkuu, aliwaahidi wachezaji wa Taifa Queens kwamba kila mmoja atapewa Sh. milioni 1, zilizobaki kutoka katika makusanyo ya gharama za maandalizi.

Alisema gharama za maandalizi zilikuwa ni Sh. milioni 158.4, lakini makusanyo yamevuka lengo kwani wamepata Sh. milioni 179.8.

"Tunawaomba wachezaji mcheze kwa kujituma, mbakishe kombe hapa nyumbani kila mmoja atapata Sh. milioni 1," alisema mama Tunu, na kuongeza kwamba wanamini motisha hiyo itawasadia wachezaji kucheza kwa juhudi zaidi.

Mgeni rasmi wa ufunguzi wa mashindano hayo, mama Salma Kikwete, ambaye ni mke wa Rais wa Tanzania, aliwataka wachezaji kucheza kwa kujituma ili waweze kubakisha kombe nyumbani.

Alisema netiboli ni mchezo mkubwa kwa wanawake hivyo unapaswa kuheshimiwa na akawataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kuwapa hamasa wachezaji wa timu yao ya taifa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles