Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nassari, wenzake jimboni nao watishiwa kuchinjwa

5th May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari

Baada  ya Mwenyekiti wa tawi la USa River, Jimbo la Arumeru Mashariki, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Msafiri Mbwambo (36), kuuliwa kwa kuchinjwa Aprili 27, mwaka huu, jana Mbunge wa Jimbo hilo, Joshua Nassari na baadhi ya viongozi wa chama hicho, wamepokea ujumbe wa maneno kwenye simu ya kiganjani unaowatishia kuwachinja.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, wakati alipokuwa kwenye ofisi yake ya Mbunge, jimboni Arumeru Mashariki, alisema kuwa amepata ujumbe wa kumtishia kumuua na viongozi wa matawi na wengine wasio na matawi, ambao walikuwa mstari wa mbele kumpigania kupata ushindi wakati wa
kampeni.

Alisema ujumbe huo aliupata kupitia simu yenye namba 0753 211367, iliyotuma ujumbe wa kuwatisha kuwachinja viongozi wa kata, kwa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Wilaya ya Arumeru, Gadiel Mwanda, Katibu wa Wilaya hiyo, Totinan Ndonde, Mwenyekiti wa kata ya Seela Sing’isi, Simba Kimunto na aliyekuwa mkuu wa operesheni ya ushindi wake, John Mrema.

Ujumbe huo aliusoma “Tumekuona unabeba jeneza kwenye gazeti, tunakuhakikishia utabeba majeneza Arumeru Mashariki, mpaka ukimbie Ubunge na baada ya Mwenyekiti Usa (Msafiri Mbwambo) kumchinja, sasa ni Simba Kimunto muda usiojulikana, utabeba jeneza lake, Jimbo hili tutalichakaza ndani ya miezi sita, nakutakia mazishi mema ya mfululizo.”

Alisema kuwa baada ya kupokea ujumbe huo akiwa anausoma ukaingia ujumbe mwingine kwa namba hiyo hiyo ukisema, “Bado wewe na Wenyeviti Chadema kwenye kata zako,”

Nassari alisema kuwa mtu huyo asiyejulikana alituma ujumbe kwa Godbles Lema usemao, “Wewe ng’ombe samba Kimunto alikuwekea Wameru 300 kukulinda Arumeru, sasa wewe utamwekea wachaga wangapi? Kwa sababu baada ya m/kiti Usa River tunamchinja yeye”

Alisema Lema naye akiwa anatafakari ujumbe huo uliingia mwingine ukisema,” Baada ya Mwenyekiti wako wa Usa  atafuata Mwenyekiti wa kata ya Seela-Sing’isi samba Kimunto huyu amekuwa kero wilaya hii ya Arumeru wenyeviti wa jimbo hili tutakabiliana nao mwezi huu mtamzika samba Kimunto unalo la kusema”

Aidha alisema kuwa baada ya kupata ujumbe huo alifanya mawasiliano na Katibu wa Chama chake wa wilaya hiyo, Totinan Ndonde, ambaye alikwenda kituo cha Polisi cha Wilaya hiyo, kutoa taarifa na alipewa RB yenye namba USR/RB/1671/2012.

Alisema pamoja na vitisho hivyo hatarudi nyuma na ataedelea na mapambano ya ukombozi wa wananchi na anaamini uongozi wake ameupata toka kwa Mungu na sio binadamu, ndio sababu wakati wa kampeni kulikuwa na kila hila, lakini alishinda.

“Mimi naamini hata nikilindwa na mitutu ya bunduki na mabomu, bila Mungu kazi bure, hivyo kwa kuwa nina Mungu nitayashinda yote na siogopi vitisho hivi, nitaendelea kusimama imara na hii dalili kuwa tunakaribia kushinda majaribu,” alisema Nassari.

Naye Katibu wa Wilaya ya Arumeru, Totinan Ndonde alipopigiwa simu ya kiganjani kuulizwa kuhusiana na hilo, alikiri kupokea ujumbe huo wa vitisho na akatoa taarifa Polisi kwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya hiyo, John Marona na kupewa RB namba USR/RB/1671/2012.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles