Friday Feb 12, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Maofisa Ardhi watimuliwa kikaoni

7th April 2012
Print
Comments
Faustine Ndugulile

Katika hali isiyotarajiwa maofisa wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi wamejikuta wakitimuliwa kwenye kikao baada ya Wabunge na Madiwani wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kukataa taarifa waliyoitoa kuhusu Mradi wa mji mpya wa Kigamboni na kuwataka wakatafute majibu ya uhakika.

Tukio hilo limetokea juzi wakati Madiwani hao wakiongozwa na Wabunge wawili, Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Mariam Kisangi, Viti Maalumu walipohudhuria kikao maalum ya utekelezaji wa mpango wa mradi wa mji mpya wa Kigamboni iliyofanyika  katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke.

Katika kikao hicho mtoa mada alikuwa mratibu wa mradi huo, Mganga Majura, ambapo katika maelezo yake alisema mradi huo umepangwa kuwa katika awamu mbili ikiwemo mpango wa kuandaa mradi ambao umekamilika na hatua ya utekelezaji wake inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Hata hivyo, wakati akitoa mada hiyo pamoja na kuonyesha picha ya video ya jinsi mji huo utakavyokuwa, wabunge hao pamoja na madiwani walitaka  kabla zoezi hilo halijaendelea wapewe ufafanuzi wa maswali manne ikiwa pamoja na lini mradi huo utaanza, wapi utaanzia, namna ya ulipaji wa fidia na nini hatma ya wananchi wa eneo hilo.

Aliyeanzisha sakata hilo alikuwa Mbunge Ndugulile, ambapo aliponyanyuka kuchangia mada hiyo alianza kuwatuhumu watendaji wa wizara hiyo kuendesha mradi huo mwendo wa kusuasua kinyume na maelekezo ya mradi mzima.

Alisema mradi huo uliotakiwa kuanza kutekelezwa mwaka 2008 ndani ya miaka miwili,  mpaka sasa  hakuna kilichofanyika.
Ndugulile alisema badala yake wizara imezuia watu kuendeleza makazi yao kwa kipindi chote hicho na hakuna jibu sahihi linalotolewa la kuanza rasmi kwa mradi huo.

Alisema endapo maofisa hao walikuja hapo kutoa maelezo tu na sio kutoa muda kamili wa kuanza kwa mradi basi watambue hakuna kitu kitakachofanyika.

"Tumechoka na maelezo yenu, kila siku tuna mipango hii na ile, leo hapa bila ya kutueleza lini mji mpya utaanza, wapi mtaanzia na lini fidia zinaanza kulipwa, hatutawaelewa patachimbika hapa," alisema Dungulile huku akionekana kukerwa na jambo hilo.

Alisema wananchi wa Kigamboni wataendelea kuwafukuza wataalamu wote wanaofika eneo hilo bila taarifa mpaka hapo wizara itakapowapa majibu ya uhakika wa kuanza kwa mradi huo.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, alipigilia msumari kwa kusema watendaji wa wizara wana ajenda ya siri ya kuichimbia kaburi CCM  kwani baadhi yao wanakutana kwa siri na kikundi kimoja cha wanaharakati na kuwapa siri zote za mradi huo kinyume na utaratibu.

Alisema sasa madiwani wote wamechoshwa na hali hiyo na aliomba kama maofisa hao wamekuja hapo hawana majibu sahihi ya maswali yao basi warudi walipotoka wakatafute majibu au wakakutane na wanaharakati hao waendeshe mradi huo hewa.

"Leo tunashangaa mnakuja hapa kuongea na sisi madiwani, lakini tunafahamu kuna kikundi kimoja cha watu mnakutana nao na kujadiliana nao juu ya mradi huu, sisi kama madiwani na wabunge hatujui chochote, hii ni ajenda mbaya dhidi ya CCM. Hatupo tayari  kuona mnaichimbia kaburi CCM na sisi wenyewe tunaona," alisema Diwani Msawa.

Hata hivyo, diwani Anderson Chale wa Kata ya Kijichi alionekana kushangazwa na watendaji hao kuitisha kikao bila kujiandaa na badala yake wanaonyesha umahiri mkubwa wa kisiasa badala ya kazi ya utendaji waliombea ajira.

Alisema wananchi wa Temeke wamechoshwa na miradi isiyo endelevu inayofanywa na wizara hiyo kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa hiyo. Alimuomba Meya wa Manispaa hiyo, Maabad Hoja, aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao kuahirisha kikao hicho mara moja kwa sababu imeonekana maofisa hao hawakuwa na jipya.

Kauli hiyo iliungwa na Mbunge Mariam Kisangi, ambaye alifananisha mradi huo sawa na bomu linalotaka kulipuka, ambapo alionya kama hakutachukuliwa hatua ya haraka yatatokea mapigano kama yanayotokea migodini kutokana na wananchi kuishiwa na subira.

Alisema mradi huo ulipoanza wananchi wengi waliupokea kwa mikono miwli wakitarajia kupata matumaini mapya, lakini matumaini hayo yameanza kupotea kutokana na mradi huo kutoanza kama walivyoelezwa kitu ambacho wengi wao sasa wameanza kuichukia serikali yao.

"Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, najua mambo yanayotokea kule lakini nahisi na Temeke

tutashuhudia kwa sababu watu wamepoteza subira na matumaini, nyie watendaji mnawasha moto kwa uzembe wenu, tunataka haya yasitokee fanyeni kazi kwa uaminifu mkubwa," alisema Kisangi.

Alisema kimsingi wanatemeke rasilimali yao kubwa wanayotegemea ni ardhi, ikiwa ardhi hiyo inachukuliwa kiujanjaujanja hawatakubali na ndipo watakapoamua kuitetea kwa nguvu zao zote.

Hata hivyo, maofisa hao akiwemo mratibu wa mradi huo Majura hawakuweza kutoa majibu hayo, kitu kilichosababisha Meya wa Manispaa hiyo kuvunja kikao hicho na kuwaagiza maofisa hao kwenda kutafuta majibu hayo na kuyawasilisha tena kwa viongozi hao kabla ya kazi ya kuhamasisha wananchi haijaanza.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment