Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wanaotaka Wabara wasiajiriwe Z`bar washindwa

7th April 2012
Print
Comments
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismael Jussa Ladhu (CUF)

Wajumbe Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), jana wamelazimika kupiga kura ya kuamua watu wa Tanzania Bara waendelee kuajiriwa katika sekta ya utalii Zanzibar au wapigwe marufuku ili kuongeza ajira kwa Wazanzibari.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismael Jussa Ladhu (CUF), kuzuia kifungu cha kuweka utaratibu wa ajira katika sekta ya utalii  wakati Baraza lilipokaa kama kamati kupitisha vifungu vya muswada wa kurekebisha Sheria ya Utalii namba 6 ya mwaka 2009.

Jussa alisema kwamba  kifungu cha 23 (3) cha sheria kinachosema ajira katika sekta ya utalii lazima awe Mtanzania neno Mtanzania lifutwe na kuweka lazima awe Mzanzibari kwa malengo ya kulinda na kuongeza ajira kwa Wazanzibari.

Kifungu  kinasema “mtu yeyote anayefanya biashara ya utalii aliyeajiri mtu ambaye sio Mtanzania kutoa huduma, lazima apate ruhusa ya maandishi kutoka kwa waziri baada ya kumthibitishia Waziri kuwa hakuna mtu wa ndani wa kujaza nafasi hiyo.” Umesema muswada huo.

Jussa alisema kwamba sheria hiyo kuruhusu watu kutoka Tanzania bara kunufaika na ajira bila ya kuwepo udhibiti kunachagia sekta hiyo kunufaisha wageni  wakati wazanzibari wengi hawana kazi Zanzibar. Alisema kwa kuwa Zanzibar ni nchi ndogo lazima iwe na utaratibu wa kulinda ajira kwa maslahi ya wananchi wake.

Hata hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillah Jihad Hassan, alisema kwamba haiwezekani Watanzania bara kuzuiwa kunufaika na ajira Zanzibar kwa vile kitendo hicho kitakuwa kinakwenda kinyume na sheria za kazi za kimataifa.

Alisema kwamba Tanzania na Zanzibar zimeridhia mkataba wa sheria za kazi za kimataifa na haiwezekani kutunga sheria zinazokwenda kinyume na sheria hiyo hasa kwa kuzingatia Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Jihadi alisema kwamba iwapo serikali itakaribisha wazo hilo sheria hiyo italeta mgongano mkubwa katika utekelezaji wake na kutaka watanzania bara waendelee kunufaika na ajira kupitia sekta ya utalii Zanzibar.

Msimamo wa Jihadi uliungwa mkono na Waziri  wa Sheria na Katiba Zanzibar,  Abubakari Khamis Bakari, ambaye alisema kufanya hivyo kutaibua mgogoro wa kuwepo sheria mbili zinazogongana katika utekelezaji wake.

Hata hivyo,  alisema kwamba jambo la msingi ni kuwepo na kanuni ambazo zitasaidia mzanzibari kupewa kipaumbele katika utaratibu wa ajira kupitia sekta ya utalii Tanzania Zanzibar.

Kutokana na Jussa na wajumbe wengine wa CCM  kuendelea kutetea Wabara kufutwa katika ajira Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alisimama na kusema kwamba haiwezekani kuweka sheria ya kuwanyima ajira Watanzania bara wakati kuna Wazanzibari pia wananufaika na soko la ajira la Tanzania bara.

Alisema kwamba kufanya hivyo kuna weza kuibua matatizo makubwa katika sura ya muungano iwapo serikali ya muungano itaaamua kudhibiti Wazanzibari kuajiriwa katika soko la ajira la Tanzania bara.

Othman alisema kwamba wakati huu Tanzania inaelekea katika soko la pamoja la Jumiya ya Afrika Mashariki sio muafaka kuwa na sheria inayoweka mipaka ya ajira katika eneo moja la muungano wa Tanzania.

Kutokana na mvutano huo Mwenyekiti wa Baraza, Mgeni Hassan Juma, aliamua wajumbe kupiga kura  wanaotaka Watanzania bara  waendelee kunufaika na ajira Zanzibar na wale wanaopinga wabara kuajiriwa Zanzibar kwa kupiga kura ya  Ndiyo na Hapana.

Hata hivyo, matokeo ya kwanza mshindi alikosekana baada ya matokeo kufungana kwa kura 20 dhidi ya 20 na kulazimika kura hiyo kurudiwa kwa mara  ya pili na serikali kuibuka mshindi katika kura hiyo.

Kabla ya kura hiyo kurudiwa wajumbe saba waliongezeka na kufanya idadi ya wajumbe  47 lakini baada ya kupiga kura wanaotaka wabara waendelee kunufaika na ajira waliibuka washindi wakiongozwa na Baraza la Mawaziri Zanzibar.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment