Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ni kweli Jaji Warioba msikubali shinikizo

3rd May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Tume ya Katiba jana ilikabidhiwa vifaa vya kazi, vikiwamo ofisi pamoja na magari. Makabidhiano hayo yalifanywa na Katibu Mkuu Kiongozi katika hafla iliyohudhuriwa na wajumbe wa Tume, mawaziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na maofisa wengine waandamizi wa serikali akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika makabidhiano ya ofisi ambayo ni jengo jipya zima, lililosheheni vifaa vya kisasa vya ofisi kama vya kuchukua kumbukumbu (hansard), mtandao wa mawasiliano wa kompyuta, fax na simu, Katibu Mkuu Kiongozi alisema kuwa magari waliyokabidhiwa Tume ni ya kuanzia kazi na kwamba serikali ilikuwa inakamilisha kazi ya kuwapatia magari mapya 30 ambayo yatawawezesha wajumbe wa Tume kufika kila kona ya Tanzania bila matatizo kukusanya maoni ya wananchi.

Katika makabidhiano hayo imeelezwa kuwa nia ya kutoa jengo jipya linalojitegemea kwa Tume ni kuiwezesha kufanya kazi bila kuingiliana na taasisi yoyote ya umma, lakini pia kuongeza usalama na utulivu wa kazi yenyewe ya kukusanya maoni ya wananchi na kuyachambua kwa kina.

Imeelezwa pia wajumbe wa Tume ambao wanatoka nje ya Dar es Salaam watapatiwa nyumba za kuishi kwa kipindi chote cha uhai wa Tume ili kuwapa utulivu wa akili, nyumba hizo zitagharimiwa samani na serikali.

Kwa ujumla tunaziona kuwa hizi ni hatua nzuri za kuanza kazi kwa Tume. Tunakumbuka vilivyo kuwa siku akiapisha wajumbe wa Tume, Rais Jakaya Kikwete, aliahidi kuwa serikali itajitahidi kadri ya uwezo wake kuiwezesha kwa vitendea kazi ili kazi yake isikwame kwa kuwa dhima iliyoko mabegani mwake ni kubwa, na ni wajibu wa serikali na kila Mtanzania kuisaidia kutimiza wajibu huu kwa nia ya kusaidia taifa hili lipate katiba inayotokana na maoni ya watu wake ifikapo 2014.

Pamoja na kupongeza hatua hizi za mwanzo, tunajisikia furaha kwa tamko la Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, kwamba hawatafanya kazi kwa shinikizo la mtu yeyote au kikundi chochote. Tunasema hii ni kauli inayowakumbusha wajumbe wa Tume kwamba hawako katika Tume kwa niaba ya ama vyama vyao, au makundi yao mengine ya kijamii, ila ni kwa niaba ya Watanzania wote.

Hakika, isingewezekana asilani kwa Tume hii kuwa na uwakilishi wa vikundi maslahi vyote katika jamii, isingewezekana na kwa kuweli haitawezekana. Kufanya hivyo ni sawa na kutaka uwakilishi mkubwa pengine mkubwa kuliko hata ukubwa wa Bunge kwa sasa, kitu ambacho kingekwamisha kabisa ufanyaji kazi kwa sababu za wingi wa watu, mgongano wa mawazo na kwa kweli hata nyenzo za kutekeleza wajibu huo ungeweza kuwa ni changamoto nyingine kubwa na nzito katika kufikiwa kwa mwisho mwema wa kuandika katiba yenyewe.

Ni kwa maana hiyo sisi tunaichukulia kwa umakini wa hali ya juu kauli ya Jaji Warioba kama angalizo muhimu kwa wananchi, kwa makundi ya kijamii na kwa vikundi maslahi vyote kuwa kazi yao ni kupeleka maoni kwa Tume, lakini si kuishinikiza au kutumia mjumbe yeyote miongoni mwa wajumbe wa Tume kwa maslahi binafsi ya kikundi.

Sisi tunawatazama wajumbe wa Tume kama wawakilishi wa Watanzania, tunawaangalia kama kikundi kidogo cha Watanzania kilichoteuliwa kwa niaba ya Watanzania kutekeleza wajibu wao kwa niaba ya wananchi wote, ndiyo maana hatutarajii kuwa kutakuwa na nongwa kama serikali itatumia kwa busara sehemu ya kodi za wananchi kufanikisha kazi za Tume kama ambavyo imekwisha kuanza kufanya kwa kukabidhi ofisi ya kisasa na vifaa vyake vya kutenda kazi.

Mwisho, tunawaomba Watanzania wenzetu kwa ujumla wetu sasa tuelekeze mawazo na maoni yetu kwa Tume hii, tuipe ushirikiano, tuwasilishe kila aina ya dukuduku juu ya katiba tunayoitaka, ni kwa kufanya hivyo tu tutakuwa tumetimiza wajibu wetu. Haisaidii sana kupiga domo mitaani na kwenye semina na warsha za elimu kuhusu katiba kama mwisho wa yote maoni hayo hayafiki kwa Tume.

Tukumbuke, kazi ya Tume si kuibua maoni yake, ila ni kukusanya maoni ya wananchi, kuyachambua na kisha kuyawasilisha kwenye vyombo husika vya maamuzi kwamba katiba wanayoitaka Watanzania kwa mujibu wa maoni yaliyokusanywa nchi nzima ni hii. Ni kwa utambuzi huu tunaitakiwa tena kila kheri Tume ya Katiba.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles