Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba kuilalamikia Shandy CAF

12th May 2012
Print
Comments
Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga

Uongozi wa wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika, Simba, unakusudia kuwasilisha malalamiko kwa shirikisho la soka barani (CAF) kutokana na vitendo vya unyama inavyofanyiwa nchini Sudan kabla ya kurudiana na Al Ahly Shandy kesho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga, tangu Simba iwasili nchini Sudan juzi imekuwa ikifanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wenyeji wake, Shirikisho la Soka Sudan (SAF) pamoja na timu ya Al Ahly Shandy.

"Wenyeji wetu kwanza wamevunja kanuni za CAF na FIFA kwa kuisafirisha timu barabarani kwa mwendo wa masaa manne kutoka Khartoum kwenda mji wa Shandy ambao upo kilometa 170 kutoka Khartoum," ilisema taarifa hiyo.

"Na wenyeji walijua umbali wake lakini wakapanga tutoke Khartoum saa 11 jioni hali iliyopelekea timu kuingia usiku Shandy baada ya mwendo wa masaa manne.

"Mbali na suala hilo pia tutatuma malalamiko kwa timu yetu ya kuwekwa kwenye hoteli isiyokuwa na viwango vya CAF na FIFA.

"Tumewekwa kwenye hoteli ambayo haina hadhi kwa kweli," ilisema taarifa ya Kamwaga ambayo ilifananisha hoteli waliyofikia na mabweni ya wanafunzi, na kupewa vitanda 24 wakati msafara wake una watu 30.
Kutokana na ukosefu huo wa vitanda, mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alilala kwenye makochi ya mapokezi pamoja na kocha msaidizi wa makipa James Kisaka, ilisema taarifa hiyo.

Viongozi wengine wa Simba, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Mkwabi na kiongozi wa msafara, Hussein Mwamba ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, pia walikosa pa kulala na hivyo wakalazimika kwenda kulala nje ya hosteli hiyo ya Shandy.

Alisema kuwa mbali na matatizo hayo, pia baada ya kufika walicheleweshewa chakula ambapo wachezaji waliamshwa saa sita usiku kwa ajili ya kula chakula cha usiku.

Wakizungumzia hali hiyo, wawakilishi wa timu ya Shandy walidai kwamba inatokana na ukweli kuwa mji wao ni mdogo na hakuna hoteli nyingine kubwa kuliko hiyo.

Kwenye mchezo wa kesho Simba inahitaji angalau kutofugwa magoli yasiyozidi mawili ili kuingia robo-fainali ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza, kufuatia ushindi wa magoli 3-0 wa nyumbani wiki mbili zilizopita.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles