Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kikwete amlilia Balozi Kyaruzi

25th May 2012
Print
Comments
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete

Rais  Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe, kuomboleza kifo cha Balozi Vedastus Nshunju Kyaruzi ambaye aliaga dunia mwishoni mwa wiki kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba baada ya ugonjwa wa muda mfupi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilisema katika uhai wake, Balozi Kyaruzi ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 alipata kuwa Katibu Mkuu wa Vyama vya Tanganyika African Association (TAA) na Tangayika African National Union (Tanu), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa (UN), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika, Kusini mwa Jwangwa la Sahara, akiwa na Makao yake Mjini Lagos, Nigeria.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na kufadhaishwa na habari za kifo cha Balozi Kyaruzi ambaye alilitumikia Taifa na nchi nyingine kwa miaka mingi na kwa uaminifu, uadilifu na ufanisi mkubwa katika nafasi mbalimbali ambazo alipata kuzishikilia katika maisha yake.

“Nimepokea habari za kifo cha Mzee Kyaruzi kwa huzuni kubwa kwa sababu ya mchango mkubwa ambao aliutoa katika maisha yake kwenye utumishi wa taifa letu kuanzia kwenye nafasi za uongozi wa kijamii na kisiasa katika vyama vya TAA na Tanu hadi kwenye utumishi wa Serikali huru ya Tanganyika na kwenye Umoja wa Mataifa,” imesema sehemu ya taarifa ya salamu hizo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment