Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mjadala wa bajeti na `mshika mawili moja humponyoka`

24th June 2012
Print
Comments

Wanaoangalia kinachoendelea bungeni wanaweza kujiuliza, imekuwaje tumefika hapa, ambako kila aina ya kejeli na dharau, hata kwa taasisi kama Bunge?

Wakati mmoja wa wabunge kadhaa wa upinzani wakasema bajeti iliyowasilishwa ni ya kijinga! Bunge linalojadili bajeti kama ile ni la kijinga, na Rais ni dhaifu ndiyo maana anaruhusu ujinga kama ule uletwe bungeni.

Lakini kuna uwezekano wowote kuwa bajeti iliyoletwa bungeni ni ya kijinga, kuwa inatofautiana na bajeti za miaka iliyopita, zilizokuwa na busara?

Baadhi ya wabunge wa chama tawala, na hata mawaziri, wakaanza kujiuliza kama haitahitajika kwa wanaoshinda ubunge kwa tiketi ya upinzani 'kupimwa akili kabla ya kuapishwa,' kitu ambacho kinarudisha swali lile la kwanza:

Alishindaje kuanzia kura ya maoni, kampeni na uchaguzi wenyewe halafu awe na 'upungufu wa akili'? Ni wazi kuwa kejeli zote zile zilikuwa siasa na siyo udhaifu wa kufikiri, lakini kwa sababu wabunge husika hawana wasiwasi, wataeleweka vipi kwa wapiga kura wao na wananchi kwa jumla, ni wazi kuna mahali tumefika ambako hata staha inagota.

Kingine kinachojionyesha ni kuwa hasira hii haielekezwi kwa mawaziri kama ilivyokuwa kama kikao kilichopita, kuwa labda Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa amewasilisha bajeti ambayo wabunge wanaipigia kelele kama hawana akili nzuri, badala ya kuikosoa kiungwana.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanataka ujumbe ufike, na kufanya kila wanaloweza kuzuia kabisa mpango huo wa fedha usipite, na hawataki kutegemea suala la kura kwa sababu 'walio wengi watashinda' yaani wabunge wa chama tawala.

Halafu inaelekea wanampigia kelele Rais kama mtu binafsi na kiongozi wa nchi, nje ya kuwa Mwenyekiti wa chama tawala, kwani kwa upande huo wangeshindana kwa sera, na siyo tuhuma za udanganyifu, uongo.

Moja ya maeneo yaliyopigiwa kelele sana ni kuwa licha ya kuwa fedha za miradi ya maendeleo siyo nyingi kama ilivyotarajiwa, hakuna uhakikisho wowote kuwa hata hizo ambazo zimeandikwa hapo zitafikishwa.

Ilisemekana kuwa yako maeneo (wilaya, n.k.) ambako fedha zimefika kiwango cha asilimia 30 hadi mwaka ukaisha. Na miradi mingi ya maendeleo iliwekwa pembeni haina fedha kabisa.

Ukiangalia kwa karibu unakuta kuwa kinachogomba hapa siyo kuwepo sera mbili tofauti kati ya chama tawala (serikali) na upinzani, ila kuhoji kama serikali ina dhamira safi katika kile inachokifanya, na ulizo hiyo imefikia mahali inagonga kwa nyundo.

Bajeti hiyo inaendana na mantiki ambayo wabunge wengi hawataki kuiangalia machoni, licha ya kuzungumziwa katika hadhara tofauti na viongozi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu.

Hawa, hasa Cleopa Msuya na Frederick Sumaye wamekuwa wakisisitiza kuwa fedha zinatakiwa kulenga miradi kadhaa yenye ufanisi mkubwa kiuchumi, na siyo kutawanywa kwa njia ambayo inavuruga tija iliyokusudiwa, jambo ambalo limezingatiwa safari hii.

Upande mwingine wa vianzio vya mgogoro, na kimantiki inaendana na suala hilo la kuelekeza fedha katika maeneo kadhaa yenye tija na uwezekano mkubwa zaidi wa kukuza uchumi, ni tofauti kati ya uchumi wa vijijini na uchumi mkuu.

Wengi kati ya wabunge wanalenga zaidi maeneo ambayo yanahusika na mahitaji ya watu, na ahadi zilizotolewa kuhusu kufikiwa au kufanikishwa kwa viwezeshaji vya hayo mahitaji, na hayajafikiwa au yamewekwa pembeni.

Kwa vile kupanga ni kuchagua, haiwezekani kila kitu kikapangwa na kupewa fedha za kutosha kama ambavyo ni wazi wabunge wanaelekea kudai. Kanuni ya kwanza ya uchumi ni hali ya uhaba wa rasilimali; suala zima la vipaumbele na kupanga bajeti ni kupanga na kupangua.

Isitoshe, mgogoro mkubwa zaidi unaonekana katika maeneo ya ushindani wa uchumi ambako bajeti inazingatia uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara, ambako Tanzania imekuwa ikipoteza sifa kila kukicha, kuwa urasimu ni mwingi sana.

Tatizo ni kuwa urasimu mara nyingi ndiyo heshima ya watawala na wabunge kupitia kamati zao wanakutana na kuwakilisha mahitaji ya mashirika ya umma – kila moja likivuta upande wake na halina uwezo au upeo wa kukubali eti serikali haina fedha; anapotafutwa mwekezaji wanaona anawanyang'anya 'tonge mdomoni.'

Wabunge hawajawahi kuona umuhimu wa ubinafsishaji au usitishaji wa umiliki wa taasisi ya kusimamia mali za mashirika ya umma, wanadai yote hiyo ni 'hongo' tu.

Hivyo tatizo la msingi hapa ni kuwa sera haijawahi kuainishwa na kuwekwa wazi, kwa mfano kuchukua mahitaji machache na kuyapa kipaumbele, hivyo walioachwa wasishtuke.

Lakini katika uchumi ambao hauna msingi wa mali binafsi, hivyo upungufu wa aina moja au nyingine unakuwa ni biashara kwa mtu fulani, utulivu unakosekana kwa vile kila mtu anaangalia 'chungu.' Ni uhafidhina sasa unakwama.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment