Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mamlaka zitumike kuwadhibiti watumishi waovu

2nd May 2012
Print
Comments

Tanzania imekuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hayo yote yanafunikwa na matukio ya muda mfupi, hivyo kuifanya safari ya kuleta mabadiliko kuwa ngumu.

Lipo tatizo la matumizi mabaya ya fedha na mali za umma, tatizo la mipango na mikakati madhubuti ya kuinua uchumi wa nchi, lingine la ustawi na maendeleo ya jamii, misingi ya demokrasia, uongozi na utawala.

Maeneo hayo yanapoainishwa kwa ujumla wake, yanaonekana kama jambo la kawaida lililogubikwa na mazoea. Watu wanazungumza, wanajadili, wanashauri, basi!

Kwa mfano, kwa muda mrefu sasa tumekuwa katika mipango na mikakati ya kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Je, mafanikio ni yapi? Jamii inashiriki vipi katika uendelezaji wake?

Utekelezaji wa mipango ya kiuchumi kama hatua ya serikali iliyofikiwa kwa kutoa fedha zilizojulikana zaidi kama `mabilioni ya JK’ leo hii umefikia wapi? Tathimini yake inatoa majwabu gani kwa umma?

Inawezekana kwa dhati kwamba yapo mambo mema yaliyofanyika, lakini kwa kiasi kikubwa, ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuwepo vitendo vingi vinavyohujumu mipango na mikakati hiyo kiasi cha kuifanya isifanikiwe.

Mathalani fedha za miradi ya maendeleo, pamoja na uchache wake katika bajeti, bado hazijaonyesha kuleta mabadiliko, kiasi kwamba kinachoonekana sasa ni vilio visivyofikia ukomo wake kuhusu umasikini.

Matumizi mabaya ya rasilimali za umma ni eneo jingine linalokwamisha utekelezaji wa azma, mipango na mikakati ya maendeleo na ustawi wa jamii.

Viongozi waliopewa dhamana za kuutumikia umma wamekuwa mstari wa mbele kuhujumu rasilimali hizo, wakizielekeza nia zao katika kujinufaisha binafsi na si taifa. Hawana tofauti na wahujumu uchumi wa nchi.

Ndio maana matukio kama vita dhidi ya ufisadi, ukihusisha vitendo mbalimbali vya uhujumu uchumi yanajitokeza. Watu wa rika na kada tofauti wanaongoza vita dhidi ya ufisadi, ingawa kwa kupata muitikio mdogo wa raia.

Vita dhidi ya ufisadi na mafisadi vimegeuzwa kuwa jukumu la kikundi cha watu wachache, badala ya ukweli kwamba inampasa kila raia ashiriki.

Tujiulize, ni kwa sababu gani taifa linafikia hali hii na nyingine zinazofanana na hiyo? Bila shaka yapo mengi ya kujadili ili kutoa jawabu.

Uadilifu

Kukosekana kwa uadilifu miongoni mwa viongozi na watendaji wa umma ni moja ya sababu ya kukithiri kwa matatizo katika Nyanja tofauti hapa nchini.

Viongozi na watumishi wamekuwa mstari wa mbele kutosimamia wajibu na majukumu yao, badala yake wameelekeza jitihada binafsi, wakitumia rasilimali za umma kujineemesha.

Ukosefu wa uadilifu huo umekuwepo kuanzia ngazi ya chini kwenye jamii hadi kwenye taifa, ambapo unakuta viongozi kama mawaziri wa serikali wakitajwa wazi wazi kuhusika na vitendo vya ufisadi.

Hoja ya msingi ni kwamba inakuwaje taifa linafikia hatua ya kuwa na ‘lundo’ la mawaziri na watendaji wengine wa serikali wasiokuwa waadilifu? Ni mamlaka gani inayohusika kuwateuwa? Mfumo gani unaotumika kuwapata viongozi hao?

Bila shaka kwa sehemu kubwa, viongozi kama mawaziri na wakurugenzi watendaji wa halmashauri na idara za serikali, wanateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Lakini inakuwaje kila wakati wateuliwe viongozi wasiokuwa waadilifu kiasi cha kuligharimu taifa?

Kiongozi mmoja mwandamizi katika usalama wa taifa, amewahi kusema katika mahojiano huku akitaka jina lake lihifadhiwe, kwamba vyombo vinavyomshauri Rais katika uteuzi wake, vinapaswa kuwa safi ili kupendekeza majina ya watu safi katika utumishi wa umma.

Moja ya mamlaka zinazohusika kwa namna ya pekee katika mchakato wa kuwapata viongozi wa kuteuliwa na Rais ni Usalama wa Taifa.

Anasema Usalama wa Taifa unapaswa kuwa na watu walio na kiwango cha juu cha uadilifu na uzalendo, wakijiweka kando kabisa mwa njama zozote zinazoweza kuuibua hali ya kupatikana kwa viongozi wasiokuwa waadilifu.

Kwa maana kama Usalama wa Taifa watajikuta wakitekeleza wajibu wao kinyume cha misingi na maadili yao, ni dhahiri kwamba taifa haliwezi kukweka mtikisiko unaosababishwa na viongozi wasiokuwa waadilifu.

Hivyo ni jambo lililo na umuhimu wa pekee, kwamba idara hiyo iliyo na majukumu nyeti inapaswa kuendelea kusimamia maadili na misingi ya kazi hiyo kwa watumishi wake.

Zipo mamlaka nyingine ambazo hata hivyo zinaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na kuingiliwa kisiasa, ili kukwamisha utekelezaji wa majukumu yao.

Lakini inawezekana mamlaka hizo zisiingiliwe kwa maslahi ya kisiasa, isipokuwa muendelezo wa nia ovu kwa taifa, hivyo kuwa sehemu ya kuibuka na kuendelea kwa vitendo viovu.

Mamlaka hizo ni kama ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi (DPP), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Je, mamlaka hizo zinatekeleza vipi wajibu wao hasa katika kushughulikia uovu uliopo ndani ya jamii, ukiratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa na watendaji wa umma?

Kuchukua uamuzi

Mkanganyiko wa matukio yanayotokea nchini, yakiiathiri jamii yanafanywa na watu ambao kimsingi wanaweza kuchukuliwa hatua kwa kadri inavyostahili.

Inawezekana udhaifu unaonekana katika maeneo tofauti kabla na baada ya kuteuliwa ama kuchaguliwa kwa viongozi wahusika. Kwa nini inachukua muda mrefu kuwashughulikia wahusika katika kashfa tofauti hasa zinazohusika na wizi wa mali za umma?

Kwa maana hata tuhuma zinazowakabili baadhi ya mawaziri hivi sasa, huku zikionekana kuwa dhahiri baada ya kuwasilishwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, bado muda unapita pasipo jamii kuziona jitihada za kuwashughulikia.

Badala yake wahusika wameendelea na wanaendelea kuweka mazingira ya kuiaminisha jamii kwamba hawahusika kwa namna yoyote kutokana na kashfa zinazowakabili! Hawastahili kuwajibika na ikibidi kushghulikiwa!

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles