Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Zilizopanda Ligi Kuu msimu ujao zijiandae kwa ushindani

23rd April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Fainali ya 9-Bora ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inatarajiwa kuhitimishwa leo kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na hadi sasa, timu zote tatu zitakazopanda daraja na kucheza ligi kuu msimu ujao zimeshafahamika.

Hadi kufikia leo, Mgambo JKT ya Tanga, Prisons ya Mbeya na wenyeji Polisi Morogoro, ndizo timu zilizofahamika kuwa zimeshapanda ligi kuu msimu ujao baada ya kujihakikishia kuwa zitamaliza katika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa fainali hizo. Kinachosubiriwa hivi sasa ni kukamilika kwa ratiba tu ya kumalizia fainali hizo.

Sisi tunaamini kwamba, kama ubabaishaji uliepukwa na klabu hizo tatu zimepanda kabla ya ligi hiyo kumalizika leo kutokana na ubora wao uwanjani, basi ligi kuu msimu ujao itapata changamoto mpya kwa kuwa na timu kali zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo klabu kongwe za Simba na Yanga zimekuwa zikitawala kwa kupokezana ubingwa katika kila msimu.

Hata hivyo, viongozi na wanachama wa klabu zote tatu zinazosubiri tu kumalizika rasmi kwa fainali hizo ili zichukuliwe rasmi kuwa ni timu za ligi kuu wanapaswa kujizatiti zaidi na kuchukua tahadhari ya mapema kuhakikisha kwamba timu zao haziishii kuwa  wasindikizaji na kucheza kwa lengo la kupigania kubaki ligi kuu .

Viongozi wa klabu za ‘maafande’ wa  Mgambo, Prisons na Polisi Moro watapaswa kuketi na wadau wa timu zao na kupanga mikakati ya namna ya kuboresha timu zao ili ziwe na vikosi vikali zaidi, vitakavyotoa ushindani wa kweli katika ligi kuu msimu ujao.

Ni matarajio yetu na pengine ya wapenda michezo wengi kwamba kupitia timu tatu hizi mpya, msimu ujao utakuwa na ligi kuu yenye msisimko zaidi kama ilivyokuwa miaka ya 1980 na 1990; wakati ambapo klabu za Simba na Yanga zilikuwa zikipata upinzani wa kweli na mara kadhaa zilijikuta zikitema ubingwa kwa wapinzani waokama Majimaji ya Songea, Tukuyu Stars ya Mbeya, Pamba ya Mwanza na klabu za Tanga za African Sports na Coastal Union.

Sisi tunaamini kuwa timu tatu hizi za majeshi zitaingia ligi kuu kwa kishindo msimu ujao na moja kati ya klabu hizo itatwaa ubingwa kama ilivyowahi kutokea miaka ya nyuma kwa akina Bakari Tutu wa African Sports ya Tanga na John Alex wa Tukuyu Stars ya Mbeya.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Tukuyu na African Sports ziliwahi kupanda daraja na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara katika misimu yao ya kwanza tu ya kushiriki ligi hiyo yenye hadhi ya juu zaidi nchini.

Katika miaka hiyo, enzi hizo ligi kuu ya Bara ikijulikana kama Ligi Daraja la Kwanza, klabu za Simba na Yanga hazikuwa zikijihakikishia ubingwa katika kila msimu kama ilivyo sasa. Ni kwa sababu ushindani ulikuwa mkali dhidi yao kulinganisha na sasa.

Tunadhani kwamba miongoni mwa sababu kubwa za kuwepo kwa ushindani mkali na msisimko kuwa wa juu katika wakati huo na klabu nyingine kama Tukuyu na African Sports kutwaa ubingwa ni pamoja na mchakato wa kupanda kwao daraja kutoka daraja (wakati huo daraja la pili) ulikuwa wa haki zaidi.

Kwa sababu hiyo, kama timu tatu zilizopanda ligi kuu Bara zimeingia baada ya kuonyesha kiwango cha juu, na kama wachezaji wao hawatabweteka na kuridhika na mafanikio waliyopata, ni wazi kwamba watafanya maandalizi makali zaidi na kuiga morari wa wachezaji wa enzi hizo wa timu kama ya Tukuyu Stars. Hilo litasaidia kuongeza ushindani zaidi na kuifanya ligi kuu msimu ujao kuwa bora maradufu.

Tunadhani kuwa hivi sasa, kupitia timu tatu mpya zilizopanda Morogoro, klabu za Simba na Yanga zitapata upinzani mkali msimu ujao kama ilivyokuwa ‘enzi’ za kuwepo kwa Pamba ya Mwanza, Ushirika Moshi, Reli Morogoro ‘Kiboko cha Vigogo’ na Mtibwa Sugar ya akina Aboubakar Mkangwa, Kassim Issa na Mecky Maxime, ambayo ilitwaa ubingwa mara mbili mfululizo katika misimu ya 1999 na 2000. Hongera Mgambo JKT, Prisons na Polisi Morogoro.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles