Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kusuasua kwa safari za reli kwaharibu biashara

16th May 2012
Print
Comments

Hali ya biashara ndani ya kampuni ya Meli nchini (MSC) imeelezwa kuwa mbaya kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kusimama kwa safari za treni kutoka Dar es salaam kupitia Tabora hadi Mwanza.

Meneja wa Biashara na Masoko wa MSC, Obedi Nkongoki, aliyasema hayo  jijini hapa jana, ambapo alieleza kuwa uchakavu wa meli zinazomilikiwa na kampuni hiyo pia ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuathiri hali ya biashara.

Alisema tangu safari za treni kupitia reli ya kati zilipoanza kusuasua na wakati mwingine kusimama kabisa, kumeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa abiria na mizigo inayosafirishwa kwa meli kati ya Mwanza, Bukoba na Nansio wilayani Ukerewe pamoja na nchi jirani ya Uganda.

Aidha, Nkongoki,  alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa meli za abiria za MV. Clarias na MV Butiama zimesimamisha safari zake kati ya Mwanza na Nansio kutokana na uchakavu.

Alisema kuwa, injini za meli hizo zimekuwa zikiharibika mara kwa mara hali ambayo si tu imeathiri biashara, lakini pia imeongeza gharama za uendeshaji kutokana na matengenezo ya mara kwa mara.

“Kusimama kwa meli zetu hizi kwa kiasi kikubwa kumesababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotumia usafiri wa majini, na hivyo kujikuta wakilazimika kulipa nauli kubwa zaidi kwa meli binafsi hasa zinazofanya safari kati ya Mwanza na Nansio.

Hata hivyo, Nkongoki, alisema MSC imefanikiwa kuifanyia matengenezo meli ya MV Clarias, ambapo inatarajiwa kuanza safari za kuekelea Nansio wakati wowote kuanzia sasa baada ya kufanyiwa ukaguzi.

Alisema kwa upande wa MV Butiama inatarajiwa kufanyiwa matengenezo makubwa baada ya kutengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2012/2013.

Wakati huo huo, Meneja huyo wa Biashara na Masoko wa MSC amesema meli ya MV Serengeti hivi sasa inafanya kazi ya kusafirisha mizigo kutoka Mwanza kuelekea Uganda.

Alisema kuwa awali meli hiyo ilikuwa ikisaidiana na MV Victoria kusafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na Bukoba mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa Nkongoki, MV Serengeti inafanya kazi ya kusafirisha shehena ya mahindi kwenda nchini Uganda baada ya MSC kupata zabuni hiyo kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles