


Watu watano wamepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu mkazi Dodoma kwa tuhuma za mauaji ya wahamiaji haramu raia wa Ehiopia 43 yaliyotokea katika kijiji cha Chitego wilayani Kongwa, mkoani hapa.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Elinaza Luvanda, Wakili wa Serikali Godfrey Wambali, alidai kuwa, washitakiwa hao walitenda kosa hilo juni 26, mwaka huu.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 43 ya mauaji.
Aliwataja watuhumiwa kuwa ni, Vicent Saiteru Linetu (42) mkazi wa Arusha ambaye ni dereva wa Fuso lililokuwa limewapakia wahamiaji hao.
Wengine ni Esther Mohamed maarufu kama Fatuma Kisuju (33) muuza duka mkazi wa Arusha, Hamisi Saidi Salim (37) ambaye pia ni Dereva na mkazi wa Arusha, Mohamed Abdala Saidi (35) mfanyabiashara mkazi wa Arusha na
Peter Michael Simpanya (43) Kondakta wa basi mkazi wa Arusha.
Hata hivyo, Hakimu Luvanda, alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa kesi za mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.
Washitakiwa hao walirudiswa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Agosti 6, mwaka huu.
Tukio hilo lilitokea Juni 26, mwaka huu, katika kijiji cha Chitego, ambapo wahamiaji haramu 43 kutoka Ethiopia walifariki na wengine 82 kunusurika kifo kwenye kontena walilokuwemo wakiwa safarini kutoka Ethiopia kwenda Malawi.