Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Sitaki nimfundishe kazi Rais Kikwete

25th April 2012
Print
Comments

Kama ningekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wabunge ‘wakiwazodoa’ mawaziri wa serikali kwa wizi na ubadhirifu wa mali za umma, ingekuwa fursa nzuri kwangu.

Ningefanya kile ambacho umma wa Watanzania unakitarajia, ningejenga na kuimarisha imani ya wanawake na wanaume wa Tanzania kwa uongozi wangu, ningeisikiliza sauti ya umma na kutenda kwa kadri ya matakwa ya umma.

Ujasiri wa wabunge hasa walio ndani ya chama ninachokiongoza kama CCM, uliowasukuma kujenga hoja zinazoungwa mkono kuanzia Mashariki hadi Magharibi mwa nchi, Kaskazini hadi Kusini mwa Tanzania, ungenirahisishia kazi.

Baada ya kuwasikiliza wabunge nikiwa ndani ama nje ya nchi, ningetambua kwamba Tanzania na maslahi yake vina umuhimu mkubwa kwa raia kuliko mawaziri wanaotuhumiwa kwa wizi na ubadhirifu wa mali za umma.

Ningebaini kuwa hata waliposimama mbele yangu wakiwa wameshika vitabu vitakatifu siku nilipowaapisha baada ya uteuzi, wakiapa kwamba watautumikia umma kwa uadilifu, ilikuwa geresha tu, kinyume chake walipanga moyoni namna ya kuitafuna nchi!

Kwa hali hiyo, ningewasiliana na Mwenyekiti wa wabunge ambaye kwa mujibu wa kanuni na utaratibu wa chama changu kama CCM, ni Waziri Mkuu, anipe taarifa rasmi ya hoja zao.

Kwa kuipokea taarifa hiyo ikihusu kilio cha wabunge, kwamba kutokana na ushahidi tofauti usiotilia shaka, ukawasilishwa bungeni na ‘kuichafua’ serikali yangu katika uso wa kitaifa na kimataifa, nisingewafumbia macho.

Jambo la msingi na ambalo lingetokana na ukweli kwamba yaliyoainishwa hayatokani na ‘umbea’ bali ukweli ulio dhahiri, ningeridhia shinikizo la wabunge kuwataka mawaziri wajiuzulu.

Ningewapa fursa ya kujichunguza nafsi zao, wakipitia neno moja baada ya jingine, mstari mmoja hadi mwingine, aya moja hata ya mwisho na kisha taarifa nzima yenye tuhuma, wapime.

Wapime ni namna gani wameichafua serikali yangu, ile niyoapa kupitia msahafu nilioushika kwa mkono wa kulia siku nikila kiapo mbele ya Watanzania, kwamba nitailinda.

Kwa vile niliwaamini na kuwapa majukumu yanayoulenga umma, lakini wakajigeuza kuwa magwiji wa kupora mali za umma, nitashirikiana na kuwaamini kwa kiwango gani?

Ningewaambia wajitafakari na kujipima mbele ya macho ya Watanzania waliozisikia tuhuma zikitajwa bungeni, halafu waone kama wana mamlaka ya kimaadili kuendelea kulipwa mishahara na marupurupu yanayotokana na kodi za waliobiwa mali za umma yaani Watanzania.

Ningewaambia wajitafakari na kuzisikia sauti za nafsi zao, kama zinawatuma kuendelea kuitumikia serikali iliyokabidhiwa dhamana ya kuzilinda mali za umma, wenyewe wakazigeuza kuwa `shamba la bibi.’

Kufikia hapo, ningewashauri kwa kauli adilifu na ambayo wasingeweza kuikataa, kwamba wachukue uamuzi mgumu wenye maslahi kwa umma, kupokea na kuikubali barua yangu ya kuwafukuza kazi.

Kupitia kazi kubwa iliyofanywa na wabunge, ningekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nisingeruhusu wala kutoa mwanya kwa Waziri aniandikie barua ya kuomba kujiuzulu, ili iweje?

Ningechukua uamuzi wa busara wa kuwafukuza kazi mara moja, ili nizinusuru mali za umma zilizobainika kuathirika kutokana na wizi unaowahusisha mawaziri niliowaamini kwa niaba ya umma.

Kwa vile taifa lipo lipo kwenye mchakato wa kuharakisha maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake, wakati barua za kuwafukuza kazi ‘mawaziri wezi’ zikipelekwa ofisini ama bungeni walipo, ningechukua fursa hiyo kuziba nafasi hizo.

Ningetekeleza jukumu hilo kwa kuvihusisha vyombo vya ulinzi na usalama, nikisikiliza ushauri wao na kuviasa visiingie katika mtego wa kutoa maoni yasikidhi ukweli na uhalisia.

Kwa maana kuwapata watumishi wa umma kama mawaziri si mfano wa kupata kikundi cha watu wanaocheza mchezo wa kupeana fedha kila mwisho wa juma.

Kwamba mnaweza kukusanyana popote mlipo, mkaridhia nani anaanza kupokea na nani atakuwa wa mwisho, kisha uchangishaji unaendelea. Hapana!

Watumishi wa umma kama walivyo mawaziri wanapaswa kuwa waadilifu, wanaoguswa na matatizo ya nchi, wanaoumizwa na umasikini wa Watanzania na wenye nia dhahiri ya kuwezesha na kutekeleza mipango na mikakati ya kuondokana na kadhia hizo.

Lakini ningekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nisingediriki kuishia katika kuwafukuza kazi ‘mawaziri wezi’ tu, bali ningetumia mamlaka yangu kuziamuru taasisi husika zifanye uchunguzi wa kina.

Uchunguzi ambao utakapobaini mali binafsi walizojilimbikizia, zikitofautiana na kipato chao na (hata pasipo kuthibitika), kukawepo mazingira kwamba waliiba wakajilimbizia, wangeanza kuwa wateja wa mahakama.

Wangekuwa wateja wa mahakama kwa maana wangeshtakiwa ili misingi ya utawala wa kisheria ifikiwe, kisha watupwe gerezani kwa kadri chombo hicho cha kutafsiri sheria kitakavyoona inafaa watakapothibitika kuhusika na uovu huo.

Kama ningekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Muungano, ningebaini kwamba wizi wa mali za umma ni jinai, kuwaondoa `mawaziri wezi’ kusingekuwa mwisho wa vitendo hivyo.

Hivyo pamoja na mahakama kutumia uwezo wake wa kisheria, ningeanzisha mchakato wa adhabu mbadala kwa mawaziri na watumishi wa umma wanaobainika kuhusika na wizi wa mali za umma.

Wasingeishia kufungwa tu bali kupata adhabu kama kuchapwa viboko hadharani na kuporwa kila kinachobainika kwamba kimetokana na wizi ama ubadhirifu wa mali za umma.

Sitaki nisadikiwe ya kwamba ninamfundisha kazi Rais Jakaya Kikwete, la hasha. Huo ni mtazamo wangu kuhusu yaliyojiri bungeni na jinsi ambavyo ningehusika kama ningekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles