Sunday Feb 7, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Machinga 'waliojichomeka' mamilioni ya JK watoswa

23rd May 2012
Print
Comments
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani hapa umechukua maamuzi magumu ya kuwakabidhi Sh. milioni 10 zilizotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga wa jijini hapa ili kutunisha mitaji.

Fedha hizo zilichelewa kukabidhiwa kwa walengwa kwa zaidi ya miezi miwili kufuatia kuibuka kundi moja la wamachinga ambalo halikuomba na kutaka kukopeshwa.

Jumuiya ya wamachinga jijini hapa imegawanyika katika makundi mawili, la kwanza linaongozwa na Mwenyekiti Mwanzilishi wa Muungano wa Machinga Mwanza (Mumajimwa), Liberatus Kabaila na la pili  aliyekuwa Katibu mwanzilishi wa umoja huo, Moshi Maketa.

Licha ya kuanzisha Mumajimwa kwa malengo mbalimbali ikiwemo kufanya mashauriano na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya kutengewa maeneo ya kufanyia biashara, uligawanyika katika makundi mawili yanayopingana.

Hata hivyo, kundi linaloongozwa na Kabaila, lilionekana kujipanga vizuri hadi kufikia hatua ya kusajili kisheria katiba ya umoja wao na kufanya uchaguzi wa viongozi, na la Maketa halikujishughulisha na maendeleo yoyote ya muungano wao.

Februari 5, mwaka huu, wakati wa kilele cha maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 35 yaliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kundi la wamachinga linaloongozwa na  Kabaila lilijitokeza na kusoma risala mbele ya Rais Kikwete  na kutoa ombi la kuwezeshwa kiuchumi ili kuendeleza biashara zao.

Ombi hilo lilikubaliwa  na Rais Kikwete kwa kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedhakupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza chini ya uratibu wa UVCCM.

Baada ya ahadi hiyo kundi la Maketa, likaibuka na kutaka kuhusishwa katika mgawo wa fedha hizo kwa madai kuwa ni wanachama halali wa Mumajimwa.

Ijumaa iliyopita, ilimlazimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, kuitisha kikao baina ya makundi hayo hasimu,  hatimaye alitoa maelekezo kwa UVCCM kufanya vikao zaidi ili kupata mwafaka kati ya pande hizo mbili.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment