Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

`Mchumba kapata kazi, lakini nikimpigia simu hataki kupokea`!

27th May 2012
Print
Comments

Mpenzi msomaji, Leo tujadili hoja kwamba mtu anapata kazi hivyo kumlazimu kuwa mbali na ama mpenzi wake, mchumba au hata familia yake. Lakini baada ya kuondoka husahau yote yaliyopita na kwenda kuanza mahusiano mapya huko aendako.

Hali hii imetokea hata kwa wale wanaopata kozi za ulaya wengine wamewatosa wake zao au waume zao, wengine wamesahau hata wazazi wao baada ya maisha mapya ya ughaibuni kuwakolea. Hebu tulijadili hili huku tukitupia jicho kisa kilichompata mwenzetu kama ujumbe wake hapa chini unavyojieleza.

Yeye anauliza swali na kuomba ushauri afanyeje; anasema; “Aunty mimi Ally wa DSM nimekuwa na mchumba tokea 2002. Sasa kapata kazi huko Serengeti hapokei simu yangu. Naomba niweke hewani nisikilize wadau wananiambiaje?”.

Naam. Msomaji huyu anataka ushauri afanyeje. Hapa lipo pia suala la ‘fimbo ya mbali haiui nyoka’. Bibie huko pengine kashapata wa karibu yake na kusahau yule wa mbali waliyesota pamoja. Hili naachia wasomaji watoe maoni na ushauri kwa ndugu yetu huyu.

Wakati tunasubiri maoni hayo, hebu turejee maoni ya wasomaji wetu waliyotuma kupitia ujumbe mfupi kwenye simu ya kiganjani kuhusu mada zilizopita.

Mmoja anazungumzia mada ya ‘mke anayemsaliti mumewe kwa kuchat na mabwana’ na kusema;

“naona huyu mwanaume asishirikiane kimapenzi na mkewe kwa sababu ya hali ya sasa ya magonjwa. Pili amrudishe kwa wazazi wake mpaka atakapojirekebisha, halafu wakapime ndipo amrudishe kama mzima(Mimi J.J , Iringa)

Mwingine anaanza sms yake namna hii, “kwa usalama wangu jina na namba yangu usitaje.

Huyo bwana anayesalitiwa na mkewe ni bora amsamehe tu cha kufanya ni muhimu akapime afya yake kama ni safi asishirikiane naye tendo la ndoa kama mimi nifanyavyo leo ni miaka 15 sitaki ushirika naye kila mara nabamba sms chafu ukimkanya anakwambia nisamehe. Dawa asitende nae huyo mke atapata anachokitafuta.(msomaji mzuri wa safu hii).

Msomaji mwingine anasema, “Nampa pole sana huyu jamaa. Hivi kumbe na wanawake wapo. Nilidhani ni wanaume tu. Mie sasa nimechoka kabisa maana mume wangu hata mazungumzo hakuna tena ndani ya nyumba yeye ni kuchat tu. Hata usiku wa manane hadi kero.

Msomaji mwingine anasema; Kwa kweli mwanamke ndio tatizo kufikia hatua ya kuficha simu siyo mwaminifu kabisa ikibidi mpeleke kwa wazee, ikishindikana mpeleke kwa viongozi wa kanisa wamuonye nadhani hawa watu wa Mungu atawasikiliza na kujirekebisha. Ikishinikana angalia sehemu ya kutokea ili kunusuru maisha yako kijana mwenzangu(Ni John Mushy wa Nzega, Tabora)

USHAURI KWA RUTTA

Mmh, kwa kumshauri Rutta, ni kwamba bado ni vijana wadogo kujiingiza kwenye mapenzi! Naona hata huyo binti bado hajui maana ya mapenzi. Unajua mapenzi siyo kukurupuka na kuanza kukutana kimwili bila kukutana malengo ya baadaye. Kwa uzoefu wangu vijana wa sasa wanawaza ngono zaidi kuliko maisha ya ndoa.

Angalia huyo binti yuko na Rutta lakini sms za uwongo kwa mwingine bila kujua madhara yake. Kwa Rutta asiwazie tena huyo binti na fedha alizompa binti achukulie kaibiwa. Ajipange upya kimaisha kwa maendeleo yake na kumuomba Mungu atapata mke mwema(Mama Lulu Kitunda, Dar).

Msomaji mwingine anasema “ Pole sana. Usikate tamaa kiasi hicho, hiyo haikuwa bahati yako. Mbona hata mimi yalinikuta kama hayo lakini sijakata tama? Mungu atakupa mwingine.(msomaji)

Kuhusu makala iliyohusu wanaume wa Moshi, yupo msomaji anayechangia kwa kusema; “wanaume wa Moshi ni balaa, hakuna familia itokayo Moshi isiyojua hivyo. Tunaishi nao kwa kuwa hatuna jinsi tumeshazaa bila hivyo, mmh tungeshatimua wengine. Haya ndio maisha(msomaji wa Moshi).

Mpenzi msomaji, mambo ya mahusiano katika familia zetu ni mengi sana na yamesababisha mitafaruku mingi wakati mwingine pasipo sababu. Na kibaya zaidi vurugu hizi husababishwa na ama mwanaume au mwanamke, kijana au msichana kutegemeana na wahusika na mazingira wanayokutania.

Leo nilitaka tu kuleta hapa ujumbe toka kwa wasomaji waliochangia mada mbalimbali kwa kutoa ushauri na maoni huku wengine wakieleza visa vyao.

Wiki ijayo nitazungumzia jinsi watu wanavyotafuta wachumba na changamoto wanazokumbana nazo nikitolea mfano mazungumzo niliyonasa toka kwa familia mbili kuhusu jinsi walivyoanza hadi kujikuta sasa ni baba na mama watoto. Usikose kionjo hicho msomaji wangu.

Hata hivyo, kama nawe unacho kisa kilichokukuta wewe kuhusu mahusiano au kilimsibu ndugu au rafiki yako, usisite kunitumia tujadili kwa pamoja. Ukiwa tayari kuwa huru kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com

.Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.

Wasalaam.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment