Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wasomi watakiwa kutoa elimu ya Katiba

3rd July 2012
Print
Comments
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe

Wanavyuo nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya kwa ajili ya mustakabali wa taifa.

Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alikuwa ni mwenyekiti katika kongamano la katiba lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na Umoja wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso).

Alisema wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini wanawategemea wasomi hao ili kuwapatia elimu sahihi kuhusu sababu ya kuundwa kwa katiba mpya huku wakiwaonyesha mapungufu yaliyopo kwenye katiba iliyopo na umuhimu wa mabadiliko hayo.

“Ni aibu kubwa kwa msomi kama mzazi wako anakuuliza kwanini tunahitaji katiba mpya, halafu huwezi kumpatia majibu sahihi. Unahitajika kumjibu kama mwenye uelewa,” alisema Mwakyembe na kuongeza:

“Kuna tofauti kati ya hoja za msomi na asiyesoma. Msomi hoja zake zinatokana na utafiti, uchambuzi na zenye kuibua hoja.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, aliwataka wanavyuo hao kuandika maoni yao kuhusu marekebisho ya katiba mpya kwa tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya kwa kuwa maandishi yana nguvu kuliko maneno matupu kwenye mikutano.

Naye, Mwenyekiti wa Tahliso, Paul Makonda, akizungumza katika kongamano hilo ambalo lilikusanya waanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini, aliwataka wasomi wenzake kuweka itikadi za vyama pembeni na kudai katiba yenye mustakabali wa maendeleo ya taifa kwa miaka 50 ijayo.

Kongamano hilo ambalo kwa mujibu wa  Dk. Mwakyembe, ni darasa kwa ajili ya kuwajengea uelewa wanavyuo kuhusiana na mabadiliko ya katiba mpya litaendelea leo huku likitarajiwa kuhudhuriwa na mwenyekiti wa tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya, jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Isaya Kisimbilu na Winfrida Kanyika, SJMC

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment