


.jpg)
Kocha Mkuu wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic, amesisitiza kuwa anaudai uongozi wa Yanga zaidi ya Dola za Marekani 15,000 (Sh. Milioni 24) na tayari anatarajia kufikisha rasmi malalamiko yake hayo katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefahamika.
Hata hivyo, jana mchana, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, aliitisha mkutano kwa vyombo vya habari vichache (NIPASHE haikualikwa) kukanusha madai ya kocha huyo, jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa maelezo ya Papic.
Akizungumza na gazeti hili, Papic alisema kuwa mkataba wake na Yanga unamalizika leo (Aprili 24) na hataweza kuendelea kuifundisha timu hiyo kutokana na kutomlipa mshahara wake na vilevile kutozungumzia hatma yake.
Papic alisema kuwa mara ya mwisho, Yanga ilimlipa kiasi cha dola za Marekani 1,000 Februari 6 mwaka huu na tangu hapo, hajalipwa kiasi kingine chochote cha fedha.
"Na hata ninapowapigia simu mwenyekiti (Lloyd Nchunga), Katibu Mkuu (Mwesigwa) wote hawataki kuzungumza lolote na mara nyingi huwa hawapokei simu wakati ninapowapigia," alilalamika kocha huyo.
Papic aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, ameamua kwenda kueleza tatizo lake hilo kwa TFF huku pia akitaka nakala ya malalamiko ya madai yake iende katika Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na la Dunia (FIFA).
Alisema vilevile kuwa kutokana na hali hiyo, anajiandaa kurejea kwao Serbia huku akiamini kwamba Yanga itaingia kwenye matatizo kutokana na kulifikisha jambo hilo kwenye mahakama ya soka inayotakiwa.
"Nimewasiliana na (Sunday) Kayuni (Kaimu Katibu Mkuu wa TFF) ili kufikisha malalamiko yangu, ila ameniambia nisubiri, atanipigia simu na sasa ndio nasubiri," alisema Papic wakati akizungumza na NIPASHE jana mchana.
Aliongeza kuwa anashangazwa na kauli hizo za Yanga zinazodai kwamba haidai kiasi chochote na wakati wanafahamu ukweli na kusema vilevile kuwa kibali chake cha kufanya kazi hapa nchini kinamalizika leo.
"Hawanitendei haki, ina maana mimi ni muongo… siwezi kufanya kitu kama hicho," aliongeza Papic.
Inaelezwa kuwa jana mchana, Mwesigwa katika mkutano wake, alisema kuwa Yanga haidaiwi kiasi chochote cha fedha na kocha huyo na mkataba wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa msimu huu.
Mwesigwa alisema vilevile kuwa endapo Papic atashindwa kuendelea kuifundisha timu yao, watamchukulia hatua za kisheria kwa sababu atakuwa amekiuka makubaliano yaliyopo kwenye mkataba ambao pande hizo mbili zilisaini.
Taarifa zaidi kutoka Yanga zinasema kuwa timu yao ilitarajiwa kuondoka wakati wowote kuanzia jana jioni kuelekea mkoani Arusha ambapo kesho watacheza mechi yao ya kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kucheza dhidi ya 'maafande' wa JKT Oljoro.