Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanawake wa kimasai walia na mila kandamizi za kiuchumi

27th April 2012
Print
Comments

Ngorongoro ni moja ya wilaya tajiri kwa raslimali inayokaliwa na jamii ya kimasai pengine kuliko wilaya yeyote mkoani Arusha ulioko kaskazini mwa Tanzania.

Wilaya hiyo ina bonde maarufu la Ngorongoro ambalo linatembelewa na watalii wanaofikia 520,000 kwa mwaka na kulipa  dola za kimarekani zipatazo  milioni 60 hivi, sawa na shilingi bilioni 94.2 kwa mwaka.

Mbali na bonde hilo, Ngorongoro pia ina kitalu cha uwindaji wa kitalii cha Loliondo ambacho kimsingi ni cha kwanza kwa ukubwa na utajiri wa wanyama nchini Tanzania.

Ngorongoro pia ina madini ya vito ambayo yanavutia wawekezaji wengi. 

Pamoja na utajiri wote huo, wananchi wake hususani wanawake wanatajwa kuwa ni maskini pengine kuliko wenzao wa maeneo mengine ambayo hayana hata robo ya utajiri uliopo huko.

Sababu za umaskini huo, unaowakabili wanawake wa Ngorongoro ni nyingi, lakini wenyewe wanaamini kuwa mila potofu za kimasai ambazo haziwapi wanawake fursa za kushiriki katika masuala ya umiliki mali.

Nairri Parakwo, ni mwanamke mkazi wa kijiji cha Ololosokwan anayetoa siri ya wao kuwa maskini wakati wa warsha ya haki ya kumiliki ardhi kwa wanawake wa jamii za kifugaji iliyoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Ujamaa Community Resources Team (UCRT).

“Kwa mila zetu wanawake tumenyimwa fursa ya kumiliki chochote. Hakuna mwanamke hata mmoja anayemiliki kipande cha ardhi hapa kwetu jambo ambalo linasababisha hali tuliyonayo,” Nairri alisema.

Hoja hii inaweza kuwa na ukweli hasa ikizingatiwa kuwa, shughuli zote za kiuchumi kama vile kilimo, biashara, ufugaji na nyinginezo zinafanyika juu ya ardhi.

Nairi anasema kuwa, hata pale mwanamke anapolima shamba mazao yakivunwa yanakuwa mali ya mwanaume ambaye ndiyo mwenye sauti ya mwisho katika  uamuzi wa  mazao hayo.
 
“Hali hii imekwenda mbali zaidi kwani hata ukiuza mazao, maziwa ama hata shanga kwa watalii ukipata fedha jioni lazima ukazikabidhi kwa baba, tofauti na hapo unaweza kujikuta unavunja ndoa na kibaya zaidi ukishaolewa huruhusiwi kurudi kwenu,” Nairri alilalamika.

Naye Ndawasai Naitisile wa kijiji cha Malambo anatoa ushuhuda mwingine wa mila kandamizi za kimasai ambapo wao kama wanawake kuwa hawajawahi hata kushirikishwa katika masuala ya uwekezaji.

“Wilaya yetu ina wawekezaji wengi wa madini, uwindaji na upigaji picha wa kitalii, lakini hakuna mwanamke hata mmoja aliyewahi kushirikishwa na kuweka saini katika mikataba na  wawekezaji hao,” Ndawasai alisema.

Alilalamika kuwa, hata mapato yatokanayo na uwekezaji mkubwa katika wilaya hiyo yanafanyiwa maamuzi na wanaume.

Kwa ujumla Ndawasai alisema kuwa wanawake hawashirikishwi katika chombo chochote cha maamuzi kutokana na mila hizo za kimasai.

Kwa upande wao wanaume wa kimasai wanasema utamaduni wao wanamchukulia mwanamke kama chombo cha kuendeleza kizazi na kutunza familia na wala si zaidi ya hapo.

“Tunaweza kuhukumiwa hasa nyakati hizi, lakini  nasema ukweli tu kwamba wanawake kwa mujibu wa utamaduni kwetu ni chombo tu cha kuendeleza kizazi kwa maana ya kuzaa, kutunza familia na kumburudisha mwanaume” alisema Parkipuny Saibulu

Ni kwa misingi hiyo, mwanamke hakupewa nafasi ya kumiliki chochote katika jamii ya kimasai ikiwemo mali na ardhi.

“Kumfanya mwanaume wa kimasai kukubali kuwatambua wanawake kama binadamu wenye haki ya kumiliki mali ni kazi ngumu na itachukua muda mrefu kufikia lengo hilo,” Saibulu alisisitiza.

Naye Mejooli Saiteu anasema kuwa, msingi wa maisha wa jamii ya kimasai umegawanya makundi ya watu na majukumu yake na hivyo kutoka asili mwanamke amepewa jukumu la kuwa chombo cha kuleta watoto.

“Leo inaonekana ni jambo baya lakini hivi ndivyo tulivyopokea kutoka vizazi na vizazi na ndiyo maana ninyi waswahili mnatushangaa kwa kudumisha mila zetu ambazo ninyi mmeshindwa” Saiteu alisisitiza.

Kwa mujibu wa mzee huyo wa kimasai anaapa kuwa, kamwe hawatakubali kuletewa utamaduni ambao umesababisha maadili kupotea katika jamii zingine.

“Kwa ninyi huko mijini ambako mnaimba masuala ya haki za wanawake mbona tunasikia ni vurugu tupu ndoa zinavunjika watoto wanatawanyika kila mmoja na lake na hakuna heshima tena katika rika mbalimbali,” anasema.


Unyanyasaji wa kiuchumi
Unyanyasaji wa kiuchumi pengine ni aina mbaya ya unyanyasaji ambayo haizungumzwi sana kama unyanyasaji wa kijinsia.

Tangu mkutano wa wanawake wa Beijing maarufu kama ‘Beijing conference’ usawa wa kijinsia umekuwa gumzo kila kona ya dunia, ambapo mataifa mengi yamekubali kutoa nafasi sawa za uongozi na umiliki wa mali baina ya wanaume na wanawake.

Lakini picha iliyoonekana katika wilaya ya Ngorongoro inaonyesha kuwa jamii za kifugaji bado zina safari ndefu kufikia kutoa fursa sawa kwa wanaume na wanawake.

Paine Eulalia Saing’eu,  afisa anayeshughulika na dawati la jinsia katika shirika la Ujamaa Community Resources Team (UCRT) na anaamini kuwa kama wanawake wangepewa fursa ya kumiliki mali ikiwemo ardhi umaskini mkubwa unaowasumbua watu wa Ngorongoro usingekuwepo.

“Kiasili wanawake ni mashujaa wa wachumi wasioimbwa. Amini amini nakwambia dunia isingekuwa na umaskini mkubwa kama wanawake wangepewa fursa za kiuchumi sawa na wanaume tangu mwanzo,” Paine anasema.

Kufuatia unyanyasaji huo wa kiuchumi ulioshamiri katika jamii ya kimasai, UCRT imeanza mradi maalum wa kuwaelimisha wanawake wa kimasai kuanza kudai haki zao zilizokandamizwa miaka mingi.

Paine alisema kuwa mradi huo pamoja na mambo mengine unalenga kuwaelimisha wanawake haki za kumiliki ardhi, kuunda mabaraza ya wanawake yatakayokuwa na wajibu wa kudai mabadiliko katika jamii yao.

Hadi sasa jumla ya mabaraza 148 ya wanawake yameshaundwa katika wilaya ya Ngorongoro kwa msaada wa UCRT na yanatarajiwa kuwa sauti ya wanawake katika ngazi za vijiji, kata na wilaya.

Pamoja na kuwaelimisha wanawake wa kifugaji na kuunda mabaraza hayo, pia shirika hilo linawasaidia kupata ardhi na hati miliki za kisheria maeneo ambayo mwamko umekuwa mkubwa.

“Kwa mfano wilaya ya Hanang tunawasaidia wanawake wapatao 19 ambao wana ardhi zao kupata hati miliki za kisheria ili kuepuka kuporwa na wanaume katika siku za usoni, ” Paine alisema.

Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa UCRT, Simon Alakara, mradi huo ambao ni wa mwaka mmoja unatarajiwa kuwafikia jumla ya wanawake wa kifugaji wanaotarajiwa kufikia 400 katika wilaya za Ngorongoro, Simanjiro, Kiteto, Monduli, Mbulu, Karatu, Hanang, Arumeru na Longido.

Katika kutoa elimu, Alakara anasema wanakutana na changamoto nyingi ambazo wakati mwingine hawana hata majibu ya kuwapa wanawake hao wa jamii ya kifugaji.

“Wakati mwingine wanawake wanataka tuwasaidie kupata hati za ardhi wanazomiliki kwa siri ili waume zao wasijue, jambo ambalo linatuwia gumu kidogo,” alisema.

Alakara anasema kwa ujumla wanawake wa jamii za kifugaji wana changamoto nyingi katika maisha yao ya kila siku na anasisitiza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwanusuru na unyanyasaji huo wa kiuchumi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles