Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Pinda atoboa siri kutoswa mawaziri

12th May 2012
Print
Comments
  Atahadharisha watumishi wengine wakae chonjo
  Awapa rungu wananchi kuwaumbua `mchwa watu`
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa kiongozi wa Mbio hizo za Mwenge huo, ernest Mwanosa baada ya kuuwasha katika uzinduzi wa mbio hizo za mwenge kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameeleza sababu zilizomfanya Rais Jakaya Kikwete, kulivunja Baraza la Mawaziri na kulisuka upya kuwa kunalenga kuleta utamaduni mpya wa matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji zaidi.

Alisema mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yalitokana na baadhi ya mawaziri kuguswa na kashfa za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha katika wizara zao kama ilivyothibitishwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akihutubia mamia ya wananchi wa mkoa wa  Mbeya jana, wakati wa sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika mjini hapa, alisema Rais Kikwete amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kulipanga upya kwa matumaini kuwa mabadiliko hayo yataleta utamaduni mpya wa matumizi ya fedha za umma.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,Dk.Fenella Mukangala, Waziri wa Ustawi wa Jamii maendeleo ya Vijana wanawake na watoto Zanzibar, Zainab Omari, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makala, Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Gooddluck Ole Medeye, Wakuu wa mikoa mbalimbali na viongozi kadhaa wa vyama vya siasa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda ametahadharisha kuwa kwa watumishi ambao wanabainika kujihusisha na ufujaji wa fedha za umma, hakuna haja ya kusubiri wachache hao wanaoshindwa kusimamia fedha na mali za umma wakaendelea na tabia hizo, badala yake watambuliwe na kutajwa mapema ili kurekebisha nidhamu katika utendaji.

“Natumia fursa hii kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano pale mnapoona mambo hayaendi vizuri tusisubiri wachache hawa wanaoshindwa kusimamia fedha na mali za umma wakaendelea na tabia hizo na tuwatambue mapema na tuwataje mapema ili kurejesha nidhamu katika utendaji,”alisem Pinda.

Wakati wa mkutano wa saba wa Bunge uliofanyika April mwaka huu, yalijitokeza majadiliano makali yaliyotokana na taarifa ya CAG ambapo mapendekezo kadhaa yalitolewa na kuungwa mkono na wabunge kwa kutolewa rai kwamba baadhi ya mawaziri walioguswa kwa namna moja au nyingine katika taarifa hiyo wawajibishwe hali iliyomfanya Rais Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri na kuwaacha wale waliokuwa wakituhumiwa.

MADAWA YA KULEVYA

Kuhusu madawa ya kulevya, Waziri Mkuu alisema tatizo hilo bado linaongezeka kila siku ambapo taarifa zilizopo zinaoonesha kuwa  katika kipindi cha 2005/2010 Watanzania 211 walikamatwa nje ya nchi wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Alisema dawa za kulevya aina ya Heroin na kilo 149 za Coacaine zilikamatwa katika kipindi cha 2010/2012 ikilinganishwa na kiasi cha kilo 163 za Heroin na kilo 44 zilizokamatwa kwa muda wa miaka kumi iliyopita yaani 2000/2009.

Pinda alisema katika mwaka 2007/2011 jumla ya ekari 2166 za mashamba ya bangi ziliteketezwa nchini, tani 2953.7 za bangi kavu zilikamatwa zikiwahusisha jumla ya watuhumiwa 51,266 na pia kuna  watumiaji wa dawa za kuelvya kwa njia ya kujidunga wapatao 25,000.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeanzisha mchakato wa kuweka sera ya Taifa ya kudhibiti dawa za kulevya nchini ambayo itatoa muongozo wa namna ya kukabiliana na matumizi pamoja na biashara haramu ya dawa hizo.

Alisema rasimu ya sera hiyo tayari imeandaliwa na matayarisho ya kuiwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi yanaendelea, pia serikali imeanzisha mchakato wa kutunga sheria mpya ili kukabiliana kikamilifu na matumizi na biashara haramu ya dawa za kuelvya ambapo mapendekezo ya sheria hiyo mpya yameshatolewa.

AMANI NA UTULIVU
Alisema moja ya mafanikio makubwa ambayo nchi yetu inajivunia baada ya kutimiza miaka 50 ya uhuru ni kujijengea misingi imara ya amani na utulivu hivyo sote tuendelee kujenga umoja na mashikamano.

“Natumia nafasi hii kutoa tahadhari kwamba ni vizuri tusibweteke na hali ya amani tuliyojijengea kwani tumeona harakati za kutaka mabadiliko katika nchi mbalimbali duniani zinazoongozwa na wananchi wengi wao wakiwa vijana na mwisho wake haujawa mzuri unaofaa kuigwa katika nchi zetu,”alsiema Pinda.

Pinda alisema kutokana na hali hiyo tunahitaji kujifunza njia bora ya kufanya mabadiliko pale tunapoona inabidi kufanya hivyo na isiwe tu kwa ajili ya kutimiza kufanya mabadiliko ya kidemokrasia, lakini pia iwe ni ushawishi mkubwa wa kutumia fursa hizo zinazojitokeza kwa wananchi hasa vijana wa kizazi kipya.


MABADILIKO YA KATIBA
Waziri Mkuu  aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano itakayoitishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba  na kutoa maoni yao kwa uhuru na utulivu bila vikwazo vyovyote.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki kikamilifu bila ubaguzi wowote katika mchakato wa kuandika katiba mpya ili nchi yetu iweze kupata katiba itakayokidhi mahitaji ya karne hii na miaka mingine ijayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani humo, miradi yenye thamani ya Sh.bilioni 6.9 itazinduliwa katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Mwenge wa Uhuru baada ya kumaliza mbio zake mkoani Mbeya utakabidhiwa mkoani Iringa Mei 20 mwaka huu.

Hivi karibuni, Rais Kikwete alilazimika kulifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri, baada ya baadhi yao kutajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusika katika vitendo ubadhirifu wa mali za umma.
 
Pia kamati kadhaa za Bunge ziliwaelekezea vidole mawaziri kwa kushindwa kusimamia vema mali za umma, na baadhi yao kuhusika kwa namna tofauti katika upotevu na ubadhirifu wa mali hizo.

Miongoni mwa waliokuwa mawaziri ambao walifukuzwa kazi na Rais Kikwete ni Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omar Nundu (Uchukuzi), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Mustafa Mkulo (Fedha), Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Wlliam Ngeleja (Nishati na Madini).
 
Pia walikuwepo naibu mawaziri waliokumbwa na ‘fagio la chuma’ la Rais Kikwete ambao ni Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).

Hata hivyo kumekuwa na hisia na wito tofauti kuhusu utendaji kazi wa baraza la mawaziri huku wengine wakionyesha wasiwasi ikiwa utafanikisha kufikia malengo ya kuharakisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
 
Miongoni mwa walioonyesha kukerwa na utendaji kazi wa baraza la mawaziri ni wabunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa upinzani.
 
Wabunge hao walikaririwa wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, wakisema mawaziri wazembe wanasababisha ama kuhusika na  upotevu na ubadhirifu wa fedha na rasilimali za umma wanastahili kuchukuliwa hatua kali.
 
Baadhi ya wabunge walifikia hatua ya kupendekeza mawaziri wahusika wanyongwea na wengine wakisema wanastahili kunyongwa.
 
Shinikizo na hisia tofauti kwa mawaziri zinaonekana kuwastua baadhi yao, ambapo Waziri wa Utalii na Maliasili, Balozi Khamis Kagasheki, ‘ameapa’ kuwashughulikia watendaji wa chini yake ikiwa atabanika kuwa miongoni wanaostahili kunyongwa.

Kasi ya kudai Rais Kikwete alibadili Baraza la Mawaziri ilifikia hatua ya kuwepo shinikizo la Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda.
 
Mchakato wa kupiga kura hiyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge uliasisiwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ingawa baadaye ilielezwa kwamba ulianzia ndani ya kamati ya wabunge wa CCM.

Lakini Spika wa Bunge Anne Makinda, alikusudia kuukwamisha kwa maelezo kuwa, pamoja na kukidhi vigezo vya kanuni, lakini usingeweza kufikisha siku 14 kwa vile mkutano husika ulibakiza takribani siku tatu hadi kukamilika kwake.

Hata hivyo, Kamati Kuu (CC) ya CCM iliridhia azma ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya baraza hilo ambapo hata hivyo, aliwafukuza kazi mawaziri sita na naibu mawaziri wawili.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles