Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kipaumbele ni afya yangu - Profesa Mwandosya

23rd May 2012
Print
Comments
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Asiyekuwa na Wizara Maalum), Profesa Mark Mwandosya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Asiyekuwa na Wizara Maalum), Profesa Mark Mwandosya, amekataa kueleza msimamo wake iwapo atajitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais mwaka 2015 au la, akisema kwa sasa kitu anachokipa nafasi ya kwanza ni kuimarisha afya yake.

Profesa Mwandosya alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, katika hafla fupi, iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.

Mwaka 2005, Profesa Mwandosya na Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, walifika katika hatua ya mwisho kati ya makada 11 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza kuomba kuteuliwa na chama kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huo, lakini wakaangushwa na Rais Kikwete katika kinyang’anyiro hicho.

“Afya kwanza, ngoja nipone,” alisema Profesa Mwandosya akijibu swali la mmoja wa wanahabari aliyetaka kujua iwapo atajitosa katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2015.Hata hivyo, alisema kwa sasa afya yake inaendelea vizuri.

Alisema uthibitisho wa hilo ni namna hivi sasa anavyoweza kumudu kutembea bila ya kusaidiwa na mkongojo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Waziri Mwandosya alisema aliacha kutembea kwa kusaidiwa na mkongojo tangu Desemba, mwaka jana, baada ya afya yake kuimarika.

Profesa Mwandosya alilazwa nchini India kwa zaidi ya miezi minane kwa matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

Kutokana na matatizo hayo, Profesa Mwandosya akiwa Waziri wa Maji, alishindwa kuhudhuria mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka jana.

Profesa Mwandosya alisema amefurahishwa kuteuliwa katika Ofisi ya Rais kwa kuwa anapenda kufanya kazi karibu na Rais.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment